Kuhusu sifa sisi hatumthibitishii Allaah isipokuwa kwa yale aliyojisifu Mwenyewe. Ni mamoja mtu atataja jina pekee pasi na kutaja yale yanayofahamishwa nalo au sifa hiyo ikawa ni katika yale yanayofahamishwa na majina yake. Ni lazima kwetu kuiamini sifa hii juu ya uhakika wake.

Mfano wa hilo Allaah amejithibitishia Mwenyewe ya kwamba yuko juu ya ´Arshi Yake. Allaah anatuzungumzisha kwa Qur-aan ilioteremshwa kwa lugha ya kiarabu iliowazi. Kila ambaye anaijua lugha ya kiarabu anajua ni nini maana ya Istawaa (استوى) katika lugha ya kiarabu. Kwa ajili hii Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) alisema baada ya kuulizwa na mtu nini maana ya:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ‘Arshi.”[1]

 “Yuko juu namna gani?” Akamjibu kwa kusema:

“Kuwa juu kunajulikana. Namna haifahamiki. Ni wajibu kuamini hilo. Ni Bid´ah kuuliza juu ya hilo.”

Hili ndio tamko lililotangaa kwake. Kuna tamko lingine lililonukuliwa kutoka kwake kwamba alisema:

“Kuwa juu si kwamba hakufahamiki. Namna haingii akilini. Ni wajibu kuamini hilo. Ni Bid´ah kuuliza juu ya hilo.”

Tamko hili ni bora zaidi kuliko tamko lililotangulia hapo kabla. Kwa sababu neno “haingii akilini” inafahamisha kwamba ikiwa dalili zote mbili – dalili ya nukuu na dalili ya kiakili – zimeshindikana basi haiyumkiniki mtu akalizungumzia.

Huu ni mfano wa sifa ya Allaah ambayo haikupokelewa sifa kuchomolewa ndani yake. Haikupokelewa kwamba miongoni mwa majina ya Allaah ni mwenye kuwa juu/mwenye kulingana (المستوى). Lakini hata hivyo tunasema kuwa yuko juu ya ´Arshi na tunaiamini sifa hii kwa njia inayolingana Naye. Vilevile tunajua kuwa maana ya Istiwaa´ ni kuwa juu. Ni ujuu maalum juu ya ´Arshi. Haihusiani na ujuu ulioenea juu ya viumbe wote. Bali ni ujuu maalum. Kwa ajili hiyo tunasema kuhusiana na maneno Yake (Ta´ala):

اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ

“Akalingana juu ya ‘Arshi.”[2]

bi maana yuko juu na ametulia kwa njia inayolingana na utukufu na ukubwa Wake. Sio kama ambavyo mtu kwa mfano anakuwa juu ya ngamia au kiti. Kwa sababu mtu anapokuwa juu ya ngamia au kiti ni ujuu ambao mtu huyo anahitajia kile kilicho chini yake. Ama kuwa juu kwa Allaah (Jalla Dhikruh) si kwamba anahitajia. Bali Allaah (Ta´ala) ni mkwasi wa kila kitu. Kila kitu ni chenye kumuhitajia Yeye. Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) hahitajii chochote.

Yule mwenye kudai kwamba Allaah anahitajia ´Arshi ili imbebe basi amemjengea dhana Mola wake (´Azza wa Jall). Yeye (Subhhaanahu wa Ta´ala) hamuhitajii kiumbe yeyote. Bali viumbe wote ni wenye kumuhitajia Yeye.

Kadhalika tunaamini kwamba Allaah ni Mwenye kushuka kwenye mbingu ya chini ya dunia na kwamba ni ushukaji wa kihakika. Lakini ni ushukaji wenye kulingana na Allaah (´Azza wa Jall) usiyofanana na ushukaji wa viumbe.

[1] 20:05

[2] 07:54

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 13-15
  • Imechapishwa: 05/07/2019