07. Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah haimfanyi mtu kuwa muislamu

Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah imekita katika maumbile. Kunakaribia kutokuwepo kiumbe anayezozana juu ya aina hii. Ibliys, ambaye ndiye kiongozi wa ukafiri, alisema:

قَالَ رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي

“Akasema: “Mola wangu! Kwa vile Umenihukumia kupotoka.””[1]

قَالَ فَبِعِزَّتِكَ لَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ

“Akasema: “Naapa kwa Utukufu Wako! Bila shaka nitawapotosha wote.””[2]

Katika Aayah hizi amekubali utendaji kazi wa Allaah na akaapa kwa utukufu Wake. Vilevile inahusiana na makafiri wengine wote ni wenye kuikubali aina hii. Abu Lahab, Abu Jahl na wenzao katika viongozi wa kikafiri walikuwa ni wenye kuikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah pamoja na ukafiri na upotevu waliokuwa nao. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَهُمْ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ

“Ukiwauliza: “Ni nani kawaumba?” Bila shaka watasema: “Allaah.”[3]

قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُونَ

“Sema: “Nani katika mikono Yake uko ufalme wa kila kitu Naye ndiye Alindae na wala hakilindwi chochote kinyume Naye ikiwa mnajua?” Watasema: “Ni Allaah pekee.”[4]

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۚ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ ۚفَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ

“Sema: “Nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini au nani anayemiliki kusikia na kuona na nani anayemtoa aliye hai kutoka mfu na anayemtoa mfu kutoka aliye uhai na nani anayeendesha mambo? Watasema: “Ni Allaah.”[5]

Kwa hivyo tunapata kuona kuwa walikuwa ni wenye kuyakubali yote haya. Isitoshe wakati wa shida wanamtakasia maombi Allaah pekee. Walikuwa wakitambua kuwa hakuna mwengine awezaye kuwaokoa kutoka katika matatizo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kwamba waungu na masanamu yao hayawezi kuwaokoa kutoka katika maangamivu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ ۖ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ كَفُورًا

“Inapokuguseni dhara baharini hupotea wale mnaowaomba isipokuwa mnamuomba Allaah Yeye pekee. Anapokuokoeni [kwa kukufikisheni] nchikavu, mnakengeuka – na mwanaadamu daima ni mwingi wa kukufuru.”[6]

Mwenye kuamini aina ya Tawhiyd hii hawi muislamu na wala haokoki na Moto. Kwa mfano makafiri waliikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Lakini pamoja na kukubali kwao huko hakukuwafanya wakawa waislamu. Allaah aliwaita kuwa ni washirikina na makafiri. Sivyo tu bali aliwahukumu kwamba watadumu Motoni milele. Yote haya pamoja na kuwa wao wanaikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah.

Kujengea juu haya kuna waandishi wanaokosea katika ´Aqiydah pale ambapo wanafuata mfumo wa wanafalsafa. Wanafasiri Tawhiyd kwamba maana yake ni kukubali kuwepo kwa Allaah, kwamba yeye ndiye muumbaji na mruzukaji. Tunawaambia kuwa hii sio ´Aqiydah ambayo Allaah aliwatuma kwayo Mitume (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam). Makafiri, washirikina akiwemo Ibliys ni wenye kuikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Viumbe wote ni wenye kuitambua aina hii ya Tawhiyd. Mitume hawakuja kwa lengo la kuwataka watu wakubali kuwa Allaah ndiye muumbaji, mruzukaji, muhuishaji na mfishaji. Haya hayatoshi na hayaokoi na adhabu ya Allaah.

[1] 15:39

[2] 38:82

[3] 43:87

[4] 23:88-89

[5] 10:31

[6] 17:67

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mujmal ´Aqiydat-is-Salaf as-Swaalih, uk. 07-08
  • Imechapishwa: 24/05/2022