Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa tatu ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja kwa watu waliokuwa ni wenye kutofautiana katika ´ibaadah zao. Miongoni mwao kuna ambao walikuwa wakiabudu Malaika, wengine walikuwa wakiwaabudu Mitume na waja wema, wengine wakiabudu mawe na miti na wengine wakiabudu mwezi na jua. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita na hakutofautisha kati yao. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ كُلُّهُ لِلَّـهِ

“Na piganeni nao mpaka kusiweko fitina na dini yote iwe kwa ajili ya Allaah.” (08:39)

MAELEZO

Msingi wa tatu ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitumwa kwa washirikina waliokuwa wakitofautiana katika ´ibaadah zao. Kuna ambao walikuwa wakiabudu Malaika, wengine wakiabudu jua na mwezi, wengine wakiabudu, wengine wakiabudu masanamu, mawe na miti, wengine wakiabudu mawalii na watu wema.

Kibaya cha ushirikina ni kuwa watu wake sio wenye kukubaliana juu ya kuabudia kitu kimoja, tofauti na wapwekeshaji ambao mwabudiwa wao ni mmoja peke Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

أَأَرْبَابٌ مُّتَفَرِّقُونَ خَيْرٌ أَمِ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ مَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا أَسْمَاءً سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم

“Je, waungu wengi wanaofarakana ni bora [kuabudiwa] au Allaah ambaye ni Mmoja pekee, Mshindi? Hamuabudu pasi Naye isipokuwa majina mmeyaita nyinyi na baba zenu.” (12:39-40)

Katika ubatili wa shirki ni kuwa watu wake ni wenye kufarikiana katika ´ibaadah zao. Hili ni kwa sababu hawapiti juu ya msingi mmoja. Badala yake wanapita juu ya matamanio yao na madai ya wapotevu, kitu ambacho kinawafanya kufarikiana:

ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا رَّجُلًا فِيهِ شُرَكَاءُ مُتَشَاكِسُونَ وَرَجُلًا سَلَمًا لِّرَجُلٍ هَلْ يَسْتَوِيَانِ مَثَلًا ۚ الْحَمْدُ لِلَّـهِ ۚ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ

“Allaah amepiga mfano wa mtu aliyekuwa na washirika wagombanao na mtu mwengine aliyesalimika na bwana mmoja tu. Je, wanalingana sawa kwa hali zao? Himdi zote anastahiki Allaah! – bali wengi wao hawajui.” (39:29)

Ambaye anamwabudu Allaah peke yake ni kama mfano wa mtumwa ambaye anamilikiwa na bwana mmoja ambapo uwepo wake anaishi katika utulivu na amani. Mtumwa yule anajua malengo na mahitaji yake na anaishi katika raha. Upande mwingine mshirikina ni kama mfano wa mtumwa anayemilikiwa na mabwana wengi na hajui ni yupi atamridhisha katika wao. Kila mmoja katika wao ana matamanio yake. Kila mmoja katika wao anataka kitu. Kila mmoja katika wao anataka aende kwake. Ndio maana amesema (Subhaanah):

ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا رَّجُلًا فِيهِ شُرَكَاءُ مُتَشَاكِسُونَ

“Allaah amepiga mfano wa mtu aliyekuwa na washirika wagombanao… “

Bi maana anamilikiwa na watu wengi na hajui ni yupi katika wao ambaye anatakiwa kumridhisha:

وَرَجُلًا سَلَمًا لِّرَجُلٍ

“… na mtu mwengine aliyesalimika na bwana mmoja tu.”

Mtu huyu ana bwana mmoja anastarehe naye. Namna hii Allaah amepigia mfano kati ya mshirikina na ambaye anamwabudu Allaah peke yake.

Washirikina wanatofautiana katika ´ibaadah zao. Pamoja na hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita wote, pasi na kutofautisha katika wao. Aliwapiga vita waabudia masanamu, mayahudi, manaswara, wenye kuabudia moto, wenye kuabudu Malaika na waja wema, bila ya kutafautisha kati yao. Hapa kuna Radd kwa wale wenye kusema:

“Ambaye analiabudia sanamu sio kama yule ambaye anamwabudu mja mwema au Malaika, kwa sababu watu hawa wa mwanzo wanaabudu mawe na miti vitu visivyokuwa na uhai. Ama kuhusu yule anayemwabudu mtu mwema au walii, hazingatiwi ni kama ambaye anaabudia masanamu.”

Kwa haya wanachotaka kusema ni kuwa yule anayeabudia makaburi hii leo anatofautiana na ambaye anaabudia masanamu na kwa ajili hiyo wanaonelea kuwa hakufuru na wala kitendo chake hichi hakizingatiwi kuwa ni shirki na hivyo hatimaye haitojuzu kumpiga vita.

Tunasema kuwa Mtume hakutofautisha kati yao, bali alionelea wote kuwa ni washirikina. Alihalalisha damu na mali yao na wala hakufarikisha kati yao. Aliwapiga vita wale wanaomwabudu al-Masiyh ilihali al-Masiyh ni Mtume wa Allaah. Vivyo hivyo aliwapiga vita mayahudi ambao wanamwabudu ´Uzayr ambaye ni mmoja katika Manabii wao au waja wema. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita na hakutofautisha kati yao. Hakuna tofauti kati ya shirki kwa yule anayemwabudu mja mwema au sanamu, jiwe au mti, kwa sababu shirki ni kumtekelezea ´ibaadah asiyekuwa Allaah. Ndio maana anasema:

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.” (04:36)

Neno “chochote” ni makatazo ya jumla yanayokusanya kila kitu anachoshirikishwa nacho Allaah (´Azza wa Jall) wakiwemo Malaika, Mitume, waja wema, mawalii, mawe na miti.

Maneno yake mtunzi:

“Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ كُلُّهُ لِلَّـهِ

“Na piganeni nao mpaka kusiweko fitina na dini yote iwe kwa ajili ya Allaah.” (08:39)

Dalili ya kuwapiga vita washirikina pasi na kutofautisha kati yao vile wanavyoabudu ni maneno Yake (Ta´ala):

وَقَاتِلُوهُمْ

“Na piganeni nao… “

Hili linakusanya washirikina wote pasi na kumbagua yeyote. Kisha akasema:

حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ

“… mpaka kusiweko fitina… “

Neno “fitina” yaani shirki na hivyo inakuwa na maana ya kwamba kusiwepo shirki yoyote. Sentesi imeenea na inajumuisha shirki aina zote, ni mamoja iwe ni shirki kwa mawalii, watu wema, mawe, miti, jua au mwezi.

وَيَكُونَ الدِّينُ كُلُّهُ لِلَّـهِ

“… na dini yote iwe kwa ajili ya Allaah.”

Bi maana ´ibaadah zote ziwe kwa ajili ya Allaah. Asishirikishwe na yeyote yule awayae. Kwa hivyo hakuna tofauti kati ya shirki wanayofanyiwa mawalii, waja wema, mawe, miti, mashaytwaan au kitu kingine.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 18/08/2022