07. Washirikina wa leo wabaya zaidi kuliko wa kale

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Msingi wa nne: washirikina wa zama zetu ushirikina wao ni wa khatari zaidi kuliko washirikina wa kale. Washirikina wa kale walikuwa wakifanya shirki katika kipindi cha raha, wakati katika kipindi cha shida walikuwa ni watakasifu katika ´ibaadah. Ama washirikina wa zama hizi ni wenye kufanya shirki katika kipindi chote, sawa iwe ni wakati wa raha au shida. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ

“Wanapopanda merikebu [wakakumbwa na misukosuko] humwomba Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini; lakini anapowaokoa [kwa kuwafikisha salama] nchikavu, tahamaki hao wanamshirikisha.”[1]

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

MAELEZO

Shirki za waliokuja nyuma ni katika kipindi chote, wakati wa raha na wakati wa shida. Wanamshirikisha Allaah pamoja na Mitume na wengine. Bali kuna ambao wameshirikisha hata katika uola na kuamini kuwa kuna Mashaykh na waja wema ambao wana taathira katika ulimwengu na kwa watu. Hii ni akili mbovu na upotofu. Kwa hili wakawa ni waovu zaidi, wenye akili finyu kabisa na ushirikina mkubwa kuliko washirikina wa mwanzoni.

Katika msingi wa nne akaweka wazi zaidi ya kwamba washirikina wa mwanzoni walikuwa na shirki khafifu ukilinganisha na shirki za waliokuja nyuma. Shirki za waliokuja nyuma ni kubwa na mbaya zaidi. Watu wa mwanzoni walikuwa wakifanya shirki katika kipindi cha raha na wakitakasa ´ibaadah katika kipindi cha shida. Ama washirikina [wa leo] katika miji mingi ni wenye kufanya shirki katika nyakati zote, ni mamoja wakati wa raha na wakati wa shida. Ni kama mfano wa ambao wanamuabudia al-Badawiy, al-Husayn, Shaykh ´Abdul-Qaadir al-Jaylaaniy na wengineo. Ni wajibu kwa mtu kutahadhari na shirki za washirikina sawa katika kipindi cha shida na raha, ndogo na kubwa. Dalili yenye kuonyesha kuwa washirikina [wa kale] shirki yao ilikuwa katika kipindi cha raha pasi na shida ni maneno Yake (Ta´ala):

فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ

“Wanapopanda merikebu… ”

Bi maana kwenye safina.

دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“… humwomba Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini.”[2]

Bi maana walipokuwa katika bahari walikuwa ni wenye kuogopa wasije kuzama kwenye bahari na safina yao ikaja kuangamia. Hapo ndipo walikuwa wakimuomba Allaah kwa kumtakasia Yeye ´ibaadah. Wanapofika nchikavu na kusalimika ndio sasa wanarudi katika shirki zao. Amesema (Jalla wa ´Alaa) katika Aayah nyinginezo:

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ ۖ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ

“Na inapokupateni dhara baharini hupotea wale mnaowaomba isipokuwa [mnamuomba Allaah] Yeye pekee. Anapokuokoeni [kukufikisheni] katika nchi kavu, mnakengeuka.”[3]

وَإِذَا غَشِيَهُم مَّوْجٌ كَالظُّلَلِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“Na yanapowafunika mawimbi kama vivuli [kwa machafuko ya bahari], basi humwomba Allaah wakimtakasia dini Yake.”[4]

Namna hii ndio ilikuwa hali ya washirikina. Katika kipindi kizito wanamtakasia ´ibaadah Allaah na wanatambua kuwa Yeye ndiye mwenye kuokoa na kwamba hakuna mungu wa haki mwingine isipokuwa Yeye. Lakini wanapokuwa katika hali ya raha wanatumbukia katika shirki pamoja na waungu na masanamu yao.

Kuhusu washirikina wa leo shirki zao ni nyakati zote. Ni watu wasiokuwa na utambuzi wowote. Wanamuabudu Allaah katika wakati wa raha na shida. Hawana upambanuzi wowote kutokana na akili zao finyu na ujinga uliowatapakaa. Tunamuomba Allaah afya na usalama. Allaah atuwafikishe sote.

Swalah na amani zimshukie Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] 29:65

[2] 29:65

[3] 17:67

[4] 31:32

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 23/03/2023