07. Mke mwema anatakiwa kutofanya upungufu katika haki za mume

Miongoni mwa sifa za mke mwema ni kutofanya upungufu katika haki za mume wake. Anatakiwa kutilia uzito na juhudi katika kumhudumia. Zingatia juu ya hili ambalo an-Nasaa´iy amepokea katika “as-Sunan al-Kubraa”[1] kupitia kwa Huswayn bin Mihsan kutoka kwa shangazi yake ambaye ameeleza ya kwamba aliingia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutekeleza haja. Baada ya kumaliza haja yake akamwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Je, wewe una mume?” Akasema: “Ndio.” Akamuuliza: “Uko vipi kwake?” Akasema: “Ninamfanyia kila niliwezalo.” Akamwambia: “Tazama ulivyo kwake. Kwani yeye ndio Pepo yako na Moto Wako.”

Ni lini mume wa mke anakuwa ni Pepo yake na ni lini anakuwa ni Moto wake?  Hapa ni lazima kwa mwanamke kufahamu uhakika huu na jambo hili kubwa.

“Uko vipi kwake?” Una ya wajibu na wewe ni mja wa Allaah. Kuna Pepo na Moto. Allaah (´Azza wa Jall) amekuamrisha na kukuwajibishia kutimiza haki hizi za mume. Zitimize. Zitekeleze kwa njia nzuri kabisa na kikamilifu ili kumtii Allaah na kufikia Radhi Zake (Subhaanahu). Timiza wajibu wako na muombe Allaah haki zako:

“Kwani yeye ndio Pepo yako na Moto Wako.”

[1] 8913 na Ahmad (19003). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (2612).

 

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifaat-uz-Zawjah as-Swaalihah, uk. 35-36
  • Imechapishwa: 13/08/2017