Kwa mfano Suufiyyah wenzetu katika Uislamu wamo katika njia ya manaswara. Wanamuabudu Allaah, wanaipa kisogo dunia na wanawaepuka watu, lakini hata hivyo hawana elimu. Hawasomi, bali wanaidhaurau elimu. Wanawaambia watu wafanye matendo na wanaona ni vipi elimu itamshughulisha mtu na kufanya matendo. Wanaona kuwa kinachotakikana kutoka kwa watu ni kufanya matendo. Wanawapuuzisha watu na suala la kutafuta elimu, kukaa kwa wanachuoni na kuchukua elimu kutoka kwao. Wanawatuhumu tuhumu mbali mbali wale wenye kujishughulisha na kutafuta elimu na kwamba wameacha kufanya matendo. Hili ni mosi.

Pili wanasema kuwa elimu haiji kwa kusoma. Badala yake wanaona kuwa elimu inamjia mtu namna hii tu! Wanaona kuwa pindi mtu atajishughulisha na ´ibaadah Allaah atamtunukia elimu bila hata ya kujifunza. Huu ni upotofu.

Tutadhari na jambo hili. Elimu inakuja kwa kusoma. Huwezi kuifikia elimu isipokuwa njia ya kusoma kupitia kwa wanachuoni. Elimu inatangulia mbele kabla ya kuzungumza na kutenda. Imaam al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) amesema katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy:

Mlango: “Elimu inatangulia kabla ya kauli na ´amali.”

Kisha akataja Aayah ifuatayo:

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ

“Basi jua ya kwamba hapana mungu wa haki ila Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako na za waumini wanaume na waumini wanawake.” (47:19)

Kwanza unatakiwa kutambua kuwa hapana mungu wa haki ila Allaah. Hili linapatikana kwa mtu kusoma, halafu baada ya hapo ndio aombe msamaha na kutenda. Kwa hivyo ni lazima kwa mtu kusoma. Elimu ndio dalili kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´a). Allaah ameteremsha Kitabu na amemtuma Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili atuelekeze katika Njia sahihi ambayo tutapita juu yake; nayo ni elimu yenye manufaa na matendo mema.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com