Vilevile ni lazima kwa mlinganizi awe mwenye subira juu ya yale maudhi yanayomkabili. Kwa sababu ni lazima kwa mlinganizi audhiwe. Ataudhiwe ima kwa maneno au kwa matendo. Hawa hapa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) walioudhiwa kwa maneno na kwa vitendo. Soma maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

كَذَٰلِكَ مَا أَتَى الَّذِينَ مِن قَبْلِهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا قَالُوا سَاحِرٌ أَوْ مَجْنُونٌ

“Namna hiyo hawakuwafikia kabla yao Mitume isipokuwa walisema: “Mchawi au mwendawazimu.”[1]

Unasemaje kwa ambaye anajiliwa na Wahy kutoka kwa Mola wake na anaambiwa usoni mwake kwamba ni mchawi au mwendawazimu? Hapana shaka yoyote kwamba ataudhika. Lakini licha ya hivyo Mitume walisubiri juu ya yale maneno na matendo waliyoudhiwa.

Mtazame Mtume wa kwanza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye watu wake walikuwa wakimchezea shere wakati walipokuwa wakipita karibu naye kipindi alipokuwa anatengeneza rikebu akiwaambia:

إِن تَسْخَرُوا مِنَّا فَإِنَّا نَسْخَرُ مِنكُمْ كَمَا تَسْخَرُونَ فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ مَن يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ وَيَحِلُّ عَلَيْهِ عَذَابٌ مُّقِيمٌ

“Ikiwa mnatufanyia kejeli, basi nasi tunakufanyieni kejeli kama mnavyotufanyia kejeli. Mtakuja kujua nani itakayemfikia adhabu itakayomtweza na itakayemteremkia adhabu ya kudumu.”[2]

Jambo halikuishilia kumchezea shere peke yake. Bali walifikia mpaka kumtishia maisha:

قَالُوا لَئِن لَّمْ تَنتَهِ يَا نُوحُ لَتَكُونَنَّ مِنَ الْمَرْجُومِينَ

“Wakasema: “Usipoacha, ee Nuuh, bila shaka utakuwa miongoni mwa wenye kupigwa mawe.”[3]

Bi maana miongoni mwa waliouawa kwa kutupiwa mawe. Hapa anaahidiwa kuuliwa pamoja na kutishiwa kwamba wamekwishawapiga mawe wengine huku wakionyesha utukufu wao na kwamba wao wamekwishawapiga mawe wengine na kwamba yeye atakuwa mmoja katika wao. Lakini hilo halikumzuia Nuuh (´alayhis-Salaam) kutokamana na ulinganizi wake. Bali ulinganizi wake uliendelea mpaka pale Allaah alipofungua kati yake yeye na watu wake.

[1] 51:52

[2] 11:38-39

[3] 26:116

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 02/11/2021