07. Mambo yanayochengua wudhuu´


Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Mambo yanayochengua wudhuu´ ni manane:

1- Kila kinachotoka kupitia njia ya mbele au ya nyuma.

2- Kila kichafu au najisi inayotoka kwenye mwili.

3- Kutokwa na akili.

4- Kumgusa mwanamke kwa matamanio.

5- Kugusa tupu ya mbele au ya nyuma kwa mkono.

6- Kula nyama ya ngamia.

7- Kuosha maiti.

8- Kuritadi kutoka katika Uislamu – Tunamuomba Allaah Atukinge na hilo.

MAELEZO

Mambo yanayochengua wudhuu´ kwamba ni maneno ni maoni ya baadhi ya wanachuoni. Wako wengine ambao wanaona kuwa ni chini ya hapo.

1- Kila kinachotoka kupitia njia ya mbele au ya nyuma kama vile mkojo, kinyesi na kila chenye hukumu yake.

2- Kila kichafu au najisi inayotoka kwenye mwili kama vile majimaji yanayotoka kwenye kidonda na matamshi yakiwa ni mengi. Ama yakiwa ni madogo ni yenye kusamehewa.

3- Kutokwa na akili kwa kulala, kulewa au kwa kuumwa. Mwenye kupotewa na akili kisha ikamrudi basi anatakiwa kutawadha.

4- Kumgusa mwanamke kwa matamanio ni maoni ya baadhi ya wanachuoni. Mtunzi (Rahimahu Allaah) katika hili amefuata maoni ya Hanaabilah. Wako wengine waliosema kuwa hakuchengui wudhuu´. Ni jambo ambalo wanachuoni wametofautiana. Maoni ya sawa ni kwamba hakuchengui wudhuu´. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwabusu baadhi ya wakeze na wala hatawadhi tena. Kuhusu maneno Yake (Ta´ala):

أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ

“… au mmewagusa wanawake… “[1]

kinachokusudiwa ni jimaa.

5- Vilevile kugusa tupu ya mbele au ya nyuma kwa mkono kunachengua wudhuu´. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayegusa dhakari yake kwa mkono wake basi atawadhe.”[2]

Ama kuhusu Hadiyth isemayo:

“Hakika hicho ni sehemu katika kiungo chako.”

wanachuoni wamejibu kwa kusema kwamba hilo lilikuwa mwanzoni mwa Uislamu kisha likafutwa au kwamba ni Hadiyth dhaifu. Kwa sababu inapingana na Hadiyth nyingi Swahiyh ambazo zinafahamisha wudhuu´ kuchenguka kwa kugusa utupu.

7- Kuosha maiti kwa sababu mara nyingi kunapelekea kugusa sehemu za siri. Haya ni maoni ya baadhi ya wanachuoni. Jengine ni kwa sababu kunapelekea katika kudhoofika kwa sababu hiyo ni vyema zaidi mtu akatawadha ili nguvu na uchangamfu wake uweze kurudi.

8- Kichenguzi cha nane ni kutoka katika Uislamu. Atakayetawadha, akaritadi kisha akaongozwa na Allaah na kutubia, basi anatakiwa kutawadha tena upya.

Wanachuoni wengi, wakiwemo Hanaabilah (Rahimahumu Allaah), wanaonelea kuwa mambo haya yanachengua wudhuu´. Wako wengine ambao wanaona kuwa ni chini ya hapo. Wanasema hakuna dalili yoyote ya wazi inayoonyesha kuwa wudhuu´ unachenguka kwa kutokwa na uchafu na najisi mwilini. Wanaona kuwa mtu atawadhe kwa ajili tu ya usalama zaidi kama mfano wa Hadiyth:

“Yule mwenye kutapika basi atawadhe.”[3]

Kadhalika inahusiana na kumgusa mwanamke kwa matamanio na kuosha maiti. Hakuna dalili ya wazi. Kujengea juu ya haya vinakuwa vichenguzi tano. Kukisemwa kwamba kutoka katika Uislamu hakuchengui wudhuu´ hivyo vichenguzi vya wudhuu´ vinakuwa vine ambavyo vinasapotiwa na dalili za wazi. Vyengine vine kuna tofauti kati ya wanachuoni:

2- Kila kichafu au najisi inayotoka kwenye mwili.

4- Kumgusa mwanamke kwa matamanio.

7- Kuosha maiti.

8- Kuritadi kutoka katika Uislamu.

[1] 04:43

[2] Ahmad (11/647), Abu Daawuud (181), an-Nasaa’iy (163), at-Tirmidhiy (82) na Ibn Maajah (479). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (1/329)).

[3] at-Tirmidhiy (87). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (1/148).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumtaaz, uk. 67-70
  • Imechapishwa: 27/06/2018