07. Kutumia staili mbalimbali wakati wa jimaa

5- Namna ya kumwingilia

Inajuzu kwake mume kufanya naye jimaa kupitia tupu yake ya mbele kwa kutumia staili yoyote anayotaka; ni mamoja atamwingilia kinyumenyume au kimbelembele [maadamu nia ni kwenye tupu ya mbele]. Amesema (Ta´ala):

 نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ

“Wake zenu ni konde kwenu. Hivyo ziendeeni konde zenu vyovyote mpendavyo.”[1]

Bi maana vile mpendavyo. Sawa kwa kutoka kwa nyuma au kupitia kwa mbele. Kuhusu hilo kuna Hadiyth. Nitatosheka na kutaja mbili katika hizo:

1- Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia: “Mayahudi walikuwa wakisema kwamba mtoto huwa makengeza ikiwa mwanaume atamwingilia mke wake kwa kutumia staili ya nyuma yake.” Ndipo kukateremshwa:

نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ

“Wake zenu ni konde kwenu. Hivyo ziendeeni konde zenu vyovyote mpendavyo.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Ikiwa ni kwa kutumia staili ya kupitia mbele au nyuma midhali ni kwenye tupu ya mbele.”[2]

2- Ibn ´Abbaas amesimulia:

“Answaar ambao walikuwa ni watu wenye kuabudu waungu wengi. Walikuwa wakiishi na mayahudi ambao ni Ahl-ul-Kitaab. Answaar walikuwa wakiwaona mayahudi ni bora kuliko wao inapokuja katika elimu na hivyo walikuwa wakiwaiga katika matendo yao mengi. Miongoni mwa amri za Ahl-ul-Kitaab ni kwamba walikuwa hawaonelei kumwingilia mwanamke isipokuwa kwa upande mmoja tu ikiwa hii ndio stara zaidi kwa mwanamke. Answaar wakawa wameiga tendo hili. Watu hawa kutoka Quraysh walikuwa wakistarehe na wanawake kwa njia mbaya kwa kupitia kwa mbele na kwa nyuma. Pindi Muhaajiruun walipofika al-Madiynah kuna mwanamume mmoja alimuoa mwanamke wa ki-Answaar. Akafanya naye hivo ambapo mwanamke yule akamkemea na kumwambia: “Hakika sisi tulikuwa tukiingiliwa kupitia tupu ya mbele. Kwa hivyo fanya hivo na vinginevyo jitenge nami. Hayo yakamfikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo Allaah (´Azza wa Jall) akateremsha:

نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ

“Wake zenu ni konde kwenu. Hivyo ziendeeni konde zenu vyovyote mpendavyo.”

Bi maana kupitia kwa mbele au kwa nyuma. Hapo ndipo mahala pa mtoto.”[3]

[1] 02:223

[2] Ameipokea al-Bukhaariy (08/154), Muslim (04/156), Ibn Abiy Haatim (01/39) – Mahmudiyyyah na ana nyongeza yeye na al-Baghawiy katika “Hadiyth ´Aliy bin al-Ja´d (01/79/8)”, al-Jurjaaniy (440/293), vilevile al-Bayhaqiy (07/195), Ibn ´Asaakir (02/93/8) na al-Waahidiy, uk. 53, ambaye amesema:

“Shaykh Abu Haamid bin ash-Sharkiy amesema:

“Hadiyth hii ni tukufu inalingana na Hadiyth mia moja.”

[3] Ameipokea Abu Daawuud (01/377), al-Haakim (02/195), al-Bayhaqiy (07/195), al-Waahidiy katika “al-Asbaab”, uk. 52, al-Khattwaabiy katika “Ghariyb al-Hadiyth” (02/73) na mlolongo wa wapokezi wake ni mzuri. al-Haakim amesema kuwa ni Swahiyh kwa masharti ya Muslim na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 99-101
  • Imechapishwa: 04/03/2018