07. Kuthibitisha majina na sifa hakupelekei kufananisha

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Bali naamini kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Simkanushii yale ambayo Yeye Mwenyewe kajisifia na wala siyapotoshi maneno kutoka mahala pake stahiki na wala sifanyi uharibifu (al-Ilhaad) katika majina Yake na Aayah Zake.”

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) anaamini yale yanayofahamishwa na Aayah Aayah. Kwani Aayah hiyo ndio mizani katika majina na sifa zote:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye.”

katika majina na sifa Zake ingawa majina Yake yanashirikiana pamoja na majina ya viumbe katika matamshi na maana yake. Lakini hata hivyo hayafanani nayo inapokuja katika uhakika na namna yake. Ushirikiano katika tamko na msingi wa maana haupelekei ushirikiano katika uhakika na namna. Amesema (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”

Hapa kuna Radd kwa Mu´attwilah. Amejikanushia Mwenyewe wa kufanana Naye na wakati huohuo akajithibitishia majina na sifa ambayo ni usikivu na uoni. Ni dalili inayothibitisha kuwa kuthibitisha majina na sifa hakupelekei kufananisha. Maneno Yake:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye.”

Hapa kuna makanusho.

وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”

Hapa kuna mathibitisho. Amejikanushia Mwenyewe wa kufanana Naye na akajithibitishia Mwenyewe majina na sifa Zake.

Simkanushii yale ambayo Yeye Mwenyewe kajisifia – Hivo ndivo walivyofanya Mu´ttwilah.

Wala sifanyi uharibifu – Uharibifu kilugha maana yake ni kumili. Kufanya uharibifu katika majina na sifa za Allaah ni kuyapindisha kutoka katika kile yanafahamisha na kwenda katika ufahamu batili. Kwa mfano kufasiri uso kwamba ni dhati, mikono kwamba ni uwezo au ni neema na kadhalika. Huku ndio kuyapotosha maneno kuyaondosha mahala pake stahiki. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي آيَاتِنَا لا يَخْفَوْنَ عَلَيْنَا

“Hakika wale wanaozipotosha Aayah Zetu si wenye kufichikana Kwetu.”[2]

Maana ya:

يُلْحِدُونَ

“… wanaozipotosha… “

ni kwamba wanayapindisha ima kwa kuyakanusha, kama walivofanya Mu´ttwilah, au kwa kuyafananisha kwa sifa alizoumba, kama walivofanya Mumaththilah, kuyazidishia kitu ambacho hakikuthibitishwa na Allaah wala Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kuyafanya ni majina ya masanamu kama mfano wa al-Laat, al-´Uzzaa na kadhalika.

[1] 42:11

[2] 41:40

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 21/03/2021