07. Kuritadi kwa kuamini


2- Kukufuru kwa kuamini: Ni mtu aitakidi kwa moyo wake mambo yanayoutengua Uislamu. Kwa mfano mtu aitakidi kuwa swalah sio wajibu na hazina maana yoyote. Aneonelee kwamba ni kwa njia ya kupakana mafuta, kama wafanyavyo wanafiki. Matokeo yake akafanya vitendo kwa dhahiri, lakini ndani ya moyo wake haviamini. Bali anajionyesha kwa uinje tu na kutamka shahaadah mbili na moyo wake ni wenye kuyakana. Amesema (Ta´ala):

إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّكَ لَرَسُولُهُ وَاللَّـهُ يَشْهَدُ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ لَكَاذِبُونَ اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً فَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ

”Watakapokujia wanafiki wakisema: “Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Mtume wa Allaah.” – na Allaah anajua vyema kuwa hakika wewe ni Mtume Wake na Allaah anashuhudia kuwa hakika wanafiki bila shaka ni waongo. Wamefanya viapo vyao [vya uongo] kuwa ni kinga wakazuia watu na njia ya Allaah.” (al-Munaafiquun 63:01-02)

Vilevile amesema (Ta´ala):

يَقُولُونَ بِأَفْوَاهِهِم مَّا لَيْسَ فِي قُلُوبِهِمْ

”Wanasema kwa midomo yao yale yasiyokuwemo katika nyoyo zao.” (Aal ´Imraan 03:167)

Akiitakidi moyoni mwake ukafiri anakuwa kafiri. Haijalishi kitu hata kama hakufanya wala hakutamka. Haijalishi kitu hata kama kwa uinje wake akawa anafanya matendo mema kama vile swalah, jihaad, swadaqah, au maneno mazuri kama vile kutamka shahaadah, lakini hata hivyo moyoni mwake anakadhibisha hilo. Huyu ni kafiri. Hii ndio dini ya wanafiki ambao wako katika tabaka la chini kabisa Motoni. Pamoja na kuwa wanaswali, wanafunga, wanapambana jihaad, lakini ilipokuwa ndani ya nyoyo zao ni makafiri wakawa katika tabaka la chini kabisa Motoni. Kwa kuwa hawaitakidi ndani ya nyoyo zao yanayotamkwa na ndimi zao au yanayofanywa na viungo vyao katika matendo yaliyowekwa katika Shari´ah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 03/05/2018