07. Kundi lililookoka litakuwepo Shaam

45- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa ´Umayr bin Haaniy ya kwamba amemsikia Mu´aawiyah akieleza kuwa amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hakutoacha kuwepo katika Ummah wangu wenye kushikamana na amri ya Allaah. Hawatodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura na wenye kwenda kinyume nao mpaka ifike amri ya Allaah nao wako katika hayo.”

´Umayr ameeleza kuwa Maalik bin Yakhaamir amesema kuwa Mu´aadh amesema:

“Watakuwa Shaam.”

Mu´aawiyah amesema:

“Watakuwa Shaam.”

46- Hammaad bin Zayd amepokea kupitia kwa al-Jurayriy ambaye kapokea kupitia kwa Mutwarrif, kutoka kwa ´Imraan bin Huswayn ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakutoacha kuwepo katika Ummah wangu kikundi kinachopigana juu ya haki. Watakuwa ni washindi juu ya wale wenye kuwatupilia mpaka wa mwisho wao wampige vita al-Masiyh ad-Dajjaal.”

Mutwarrif amesema:

“Nimepeleleza kikundi hichi na kuona kuwa ni watu wa Shaam.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Sa´d bin Abiy Waqqaas aliyesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hawatoacha wamagharibi, Ahl-ul-Gharb, kuwa ni washindi juu ya haki mpaka kisimame Qiyaamah.”

Imaam Ahmad amefasiri wamagharibi katika Hadiyth hii ya kwamba ni watu wa Shaam. Mashariki na magharibi ni suala la kijamaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyasema haya al-Madiynah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaita watu wa Najd na wairaki watu wa mashariki, Ahl-ul-Mashriq. Kwa ajili hiyo ndio maana watu wa Shaam walikuwa wakiitwa wamagharibi, Ahl-ul-Maghrib. Vivyo hivyo walikuwa wakiita Baswrah India kwa kuwa mji huo unapatikana kuelekea India. Kwa ajili hii Khaalid alisema pindi ´Umar alipomtenga kutokamana na Shaam:

“´Umar ameniamrisha kuja India.”

Mpokezi amesema:

“India kwetu ilikuwa ni Baswrah.”

Wengine wakafasiri magharibi kama ndoo kubwa na kusema kuwa Hadiyth inawalenga waarabu kwa kuwa wao ndio wenye kuchota maji kwenye vidoo kama hivi. Haya ni maoni vilevile ya ´Aliy al-Madiyniy na wengineo.

Kumepokelewa Hadiyth nyingi zinazosimulia namna ambavyo waarabu wataangamia katika zama za mwisho na kwamba hatokubaki yeyote katika wao wakati huo isipokuwa atakuwa Shaam. Kwa hiyo tafsiri ya Hadiyth inarudi kwa watu wa Shaam.

47- Kinachothibitisha ya kwamba kundi hili litakuwa Shaam ni Hadiyth ya Mu´aawiyah bin Qurrah ambaye kaeleza kutoka kwa baba yake aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watapoangamia watu wa Shaam basi kutakuwa hakuna kheri kwenu. Hakutoacha kuwepo kikundi katika Ummah wangu chenye kunusuriwa. Hakitodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura mpaka isimame Saa.”

Ameipokea Imaam Ahmad na at-Tirmidhiy aliyesema:

“Hadiyth ni Swahiyh.”

Kuhusu yale yaliyosemwa na wanachuon – kama vile Ibn-ul-Mubaarak, Yaziyd bin Haaruun, Ahmad bin Hanbal, ´Aliy al-Madiyniy, al-Bukhaariy na wengineo – ya kwamba kundi hili ni Ahl-ul-Hadiyth, hayapingani na yale tuliyoyataja. Kwa kuwa katika zama za mwisho imani na Uislamu vitatulizana Shaam. Shaam itakuwa ndio makazi ya waumini. Kwa hivyo ni lazima ndio kuwepo mirathi ya utume ya elimu ambapo kunafikiwa uongozi wa mambo ya dini na ya dunia. Wanachuoni wa Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Shaam ni lazima wao ndio kundi lililonusuriwa lililoshikamana na haki. Wao ndio ambao hawadhuriki na wale wenye kuwakosesha nusura.

48- Ka´b-ul-Ahbaar amesema:

“Watu wa Shaam ni upanga katika panga za Allaah. Kupitia wao Allaah anawalipiza kisasi wale wanaomuasi katika ardhi Yake.”

49- ´Awn bin ´Abdillaah bin ´Utbah amesema:

“Nimesoma namna ambavyo Allaah ameteremsha kwa baadhi ya Mitume Wake: “Allaah (´Azza wa Jall) anasema: “Shaam ni podo la mshale Wangu. Pindi ninapowakasirikia watu basi Huwapiga kwa mishale yake.”

50- Qataadag amesema kuhusiana na maneno ya Allaah:

وَإِنَّ جُندَنَا لَهُمُ الْغَالِبُونَ

“Hakika jeshi Letu ndilo litakaloshinda.”[1]

“Ni watu wa Shaam.”

51- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Msiwatukane watu wa Shaam. Kwani hakika wao ndio wanajeshi wa Allaah wenye kutangulia.”

52- Kumepokelewa makatazo juu ya kuwatukana watu wa Shaam. Ya´quub bin Shaybah amepokea katika “al-Musnad” yake ya kwamba ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Msiwapige vita watu wa Shaam baada yangu.”

53- Abul-Qaasim bin ´Asaakir amepokea kutoka kwa Abu Bakr an-Nahshliy ambaye amesema:

“Nilikuwa Kuufah pindi nguvu za Shaam zilipokuja kuushambulia mji huo. Ghafla nikamsikia mzee mmoja mwenye sauti nzuri akiwa na rangi ya hina juu ya mpando wake akisema: “Ee Allaah! Usitupe ushindi juu yao. Ee Allaah! Tutenganishe na wao.” Nikasema: “Ee mja wa Allaah! Hivi wewe humchi Allaah?” Unawaona watu wamekuja kutupiga vita na kuwafanya watumwa kizazi chetu halafu wewe unasema: “Ee Allaah! Usitupe ushindi juu yao.” Ndipo akasema: “Ole wako! Mimi nimemsikia ´Abdullaah bin Mas´uud akisema: “Hakuna anayewashinda watu wa Shaam isipokuwa tu viumbe waovu.”

[1] 37:173

  • Mhusika: Imaam ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Baghdaadiy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-ush-Shaam, uk. 59-70
  • Imechapishwa: 09/02/2017