Kuhusu “Kitaab-ut-Tawhiyd”, ni moja katika vitabu bora kabisa vya Imaam na Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab. Alikitunga katika kubainisha Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah, ambayo ni kumpwekesha Allaah katika ´ibaadah na kujiepusha mbali na vyote vyenye kuabudiwa asiyekuwa Yeye, shirki kubwa yenye kuitengua au shirki ndogo yenye kuitia kasoro. Ametilia mkazo aina hii kwa sababu ndio ambayo inamwingiza mtu ndani ya Uislamu na inamsalimisha mtu na adhabu ya Allaah. Hii ndio aina ya Tawhiyd ambayo Mitume wametumilizwa nayo na vitabu vikateremshwa kwa ajili yake. Aina hii ya Tawhiyd ndio ambayo washirikina wamekwenda kinyume nayo katika kila zama na pahali.

Washirikina waliikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, lakini haikuwaingiza katika Uislamu. Wala haikuheshimisha damu na mali zao. Wala haikuwasalimisha kutokamana na Moto. Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ni dalili na hoja ya Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Ijapkuwa wasomi wa falsafa wamezichosha nafsi zao katika kuithibitisha aina hii na wakaijengea vitabu katika ´Aqiydah, lakini ni jambo liliopo. Mitume hawakufikisha Tawhiyd sampuli hii. Mitume walifikisha ujumbe wa kumwabudu Allaah pekee. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

”Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [waungu batili].”[1]

Ndio maana Shaykh akatilia bidii katika maudhui haya. Amekigawa katika milango na akaitolea ushahidi kwa Aayah na Qur-aan na Hadiyth. Kitabu kimejengwa juu ya Qur-aan na Sunnah.

Katika kitabu hiki Shaykh (Rahimahu Allaah) ametaja tu Hadiyth ambazo ni Swahiyh na nzuri au Hadiyth zilizo na cheni za wapokezi dhaifu lakini ina mapokezi yenye kuitia nguvu au inaingia ndani ya msingi wenye kuenea unaothibitishwa na Qur-aan na Sunnah. Mwishoni mwa kila mlango Shaykh hutaja faida za ki-´Aqiydah zinazopatikana kutoka katika Aayah za Qur-aan na Hadiyth. Ni jambo linamsaidia mtu kukielewa kitabu kwa njia ya kwamba msomaji anatoka kwenye kila mlango hali ya kuwa amefikia elimu nzuri.

Kwa msemo mwingine ni kwamba kitabu hiki kimejengeka juu ya Qur-aan na Sunnah, na si juu ya kanuni za kimantiki na istilahi za wanafalsafa ambazo makosa yake ni mengi kuliko kupatia kwake – ikiwa ndani yake kuna kupatia.

[1] 16:36

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 09/09/2019