Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

684- Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya chuku ilihali ni Muhrim na akafanya chuku ilihali amefunga.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy.

685- Shaddaad bin Aws (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwendea bwana mmoja al-Baqiy´ ilihali anafanya chuku katika Ramadhaan ambapo akasema: “Amefungua mwenye kuumika na mwenye kuumikwa.”[2]

Wameipokea watano isipokuwa at-Tirmidhiy. Ameisahihisha Ahmad, Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan.

686- Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mwanzoni wakati ilikuwa inachukizwa kufanya chuku kwa mfungaji Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimpitia Ja´far bin Abiy Twaalib aliyekuwa anafanya chuku ilihali amefunga ambapo akasema: “Wawili wote hawa wamefungua.”[3]

Kisha baadaye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamruhusu mfungaji kuumikwa. Anas mwenyewe alikuwa akiumikwa ilihali amefunga.

Ameipokea ad-Daaraqutwniy ambaye ameona kuwa ni yenye nguvu.

MAELEZO

Je, kufanya chuku kunafunguza au hapana? Maoni sahihi ni kwamba kuumikwa kunamfunguza yule mfanyaji na mfanywaji wote wawili. Hilo ni kutokana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Amefungua mwenye kuumika na mwenye kuumikwa.”

Katika zama zile mfanya chuku alikuwa akiivuta damu kwa bomba refu sana kiasi cha kwamba kuna khatari kukaingia kitu kinywani mwake katika damu ile. Matokeo yake akawa ni mwenye kufungua.

Kuhusu yule anayeumikwa, anafungua kwa sababu anapoteza damu nyingi ambazo zinamwathiri na kumdhoofisha mwili wake. Hivyo ikawa ni katika rehema za Allaah kwamba yule mwenye kufanyiwa chuku anafungua. Kutokana na hayo ikiwa ni funga ya lazima ni haramu kwake kufanyiwa chuku wakati wa mchana. Akilazimika kufanyiwa chuku basi itafaa kwa haja. Katika hali hiyo muumikwa anatakiwa kula na kunywa mchana uliobaki kwa sababu amekwishafungua kwa sababu ya udhuru.

[1] al-Bukhaariy (1938).

[2] Ahmad (2/122), Abu Daawuud (2369), an-Nasaa’iy (3126), Ibn Maajah (1681) na Ibn Hibbaan (3533).

[3] ad-Daaraqutwniy (2260).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mukhtaswar ´alaa Buluugh-il-Maraam (2/410-413)
  • Imechapishwa: 24/04/2020