07. Hadiyth “Ambaye atatawadha na akaeneza vizuri wudhuu´ wake… “

182 – ´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ambaye atatawadha na akaeneza vizuri wudhuu´ wake, basi huondoka madhambi yake kutoka mwilini mwake mpaka yakaondoka kutoka chini ya kucha zake.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“´Uthmaan alitawadha kisha akasema: “Nilimwona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akitawadha mfano wa wudhuu´ wangu huu. Kisha akasema: “Yule ambaye atatawadha namna hii, basi atasamehewa yale madhambi yake yaliyotangulia na swalah yake na kutembea kwake kwenda msikitini itakuwa ni ziada ya thawabu.”

Ameipokea Muslim na an-Nasaa´iy kwa ufupi ambapo tamko lake ni kama ifuatavyo:

“Hakuna mtu yeyote atakayetawadha ambapo akafanya vizuri wudhuu´ wake isipokuwa atasamehewa [madhambi] yaliyoko kati yake na swalah nyingine atakayoiswali.”

Cheni ya wapokezi wake iko kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim. Ibn Khuzaymah pia ameipokea katika “as-Swahiyh” yake kwa ufupi kama ulivyo upokezi wa an-Nasaa´iy. Aidha Ibn Maajah ameipokea kwa ufupi na ameongeza mwishoni mwake kwamba Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hata hivyo asighurike yeyote.”[2]

Katika tamko la an-Nasaa´iy imekuja:

“Yule atakayekamilisha wudhuu´ kama alivyoamrisha Allaah (Ta´ala), basi zile swalah tano zitakuwa ni kifutio cha madhambi kwa yale yaliyoko baina yazo.”

[1] Swahiyh.

[2] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim, hata hivyo imekuja kwa tamko linalosema:

”Yule ambaye atatawadha namna hii, halafu akasimama na kuswali Rak´ah mbili, basi atasamehewa yale madhambi yake yaliyotangulia.” Kisha akasema: “Hata hivyo msighurike.”

al-Bukhaariy ameipokea kwa tamko hili.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/189-190)
  • Imechapishwa: 14/04/2021
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy