07. Dalili zinahusiana na ukafiri mkubwa, na sio ukafiri mdogo

Mtu akiuliza kama kuna uwezekano ukafiri huo uliotajwa ikawa inakusudiwa kukufuru neema au kufuru ndogo, kama maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mambo mawili kwa watu ni kufuru; kutukaniana nasabu na kuomboleza juu ya maiti.”[1]

“Kumtukana muislamu ni dhambi nzito na kumpiga vita ni kufuru.”[2]

nasema kuwa si sahihi kutokana na sababu mbili:

1- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefanya swalah kuwa ni mpaka kati ya ukafiri na imani, waumini na makafiri. Mpaka unawekwa kwa ajili ya kupambanua kitu kimoja na kingine. Vitu viwili hivyo tofauti vimeachana na havikuchanganyika.

2- Swalah ni nguzo ya Uislamu. Ukafiri huu inahusiana na ule mkubwa unaomtoa mtu katika Uislamu kwa sababu amebomoa nguzo ya Uislamu. Hilo ni tofauti na ukafiri wenye kutumiwa kwa ambaye anafanya kitendo cha kikafiri.

3- Kuna dalili zengine zinazotilia nguvu kwamba ukafiri wa asiyeswali ni wa aina kubwa wenye kumtoa mtu katika Uislamu. Kwa hiyo ukafiri huu unatakiwa kufasiriwa kwa mujibu wa dalili zengine ili ziafikiane.

4- Ibara mbili hizo za maandiko zinatofautiana. Inapokuja kwa kuacha swalah Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Baina ya mtu na shirki na kufuru ni kuacha swalah.”

Ameitaja kufuru kwa fomu ya uhakika ikifahamisha kwamba inahusiana na ukafiri wa kweli tofauti na ukafiri uliotajwa kwa fomu isiyokuwa ya kihakika au kwa fomu ya kitendo. Katika hali hiyo kitendo hicho kinakuwa ni katika kufuru au kwamba kufuru ni katika kitendo hicho kitu, na sio ukafiri ulioachiwa ambao unamtoa mtu katika Uislamu.

[1] Muslim (67).

[2] al-Bukhaariy (48) na Muslim (64).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Hukm Taarik-is-Swalaah, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 22/10/2016