07. Dalili ya tano kutoka katika Sunnah kwamba Allaah yuko juu ya viumbe

5- Abul-Fath ametuhadithia: Abul-Fadhwl Ahmad bin al-Hasan bin Khayruun ametuhadithia: Abu ´Aliy al-Hasan bin Ahmad bin Ibraahiym bin Shaadhaan ametuhadithia: Abu Sahl Ahmad bin Muhammad Ziyaad al-Qattwaan: Abu Yahyaa ´Abdul-Kariym bin al-Haytham bin Ziyaad ad-Dayr´aaquuliy ametuhadithia: Rajaa’ bin Muhammad al-Baswriy ametuhadithia: ´Imraan bin Khaalid bin Twaliyq ametuhadithia: Baba yangu amenihadithia, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake aliyesema:

“Quraysh walizozana kwa al-Husayn, baba yake na ´Imraan, na wakasema: “Mwanamume huyu anawatukana waungu wetu. Tunataka uongee naye na umuwaidhi.”Wakatembea naye mpaka walipokaribia kufika katika mlango wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakakaa na al-Husayn akaingia ndani. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuona na akasema: “Mpeni nafasi mzee.”Wakafanya hivo. ´Imraan na Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio walikuwepo hapo. al-Husayn akasema: “Tumefikiwa na khabari kwamba wewe unawatukana waungu wetu. Baba yako alikuwa mtu mtukufu.” Akasema: “Baba yangu mimi na baba yako wewe wako Motoni. Ee Husayn! Ni waungu wangapi unaoabudu hii leo?”Akasema: “Saba ardhini na mmoja yuko mbinguni.” Mtume akasema: “Unapofikwa na matatizo ni nani unayemuomba?” al-Husayn akajibu: “Ni Yule aliye mbinguni.”Mtume akasema: “Anakujibu pekee na unamshirikisha na wengine? Ima huko radhi Naye au huchelei akuadhibu.” Akasema: “Hakuna hata moja katika hayo mawili.”Nikatambua kuwa sijawahi kuongea na mtu mfano wake. Akasema: “Ee Husayn! Ingia katika Uislamu utasalimika.” Akasema: “Mimi nina watu na familia walio chini yangu. Niwaambie nini?”Akasema: “Waambie:

“Ee Allaah! Ninakuomba uniongoze kwa yale yaliyo na kheri na mimi, unilinde kutokamana na shari ya nafsi yangu, nifundishe yatayonifaa, uninufaisha na yale Uliyonifunza na Unizidishie elimu itakayonifaa.”

Akasema hivo na hakuwahi kusimama mpaka akawa ameshaingia katika Uislamu. Hivyo ´Imraan akabusu kichwa chake, mikono yake na miguu yake. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoyaona hayo akaanza kulia. Kukasemwa: “Ee Mtume wa Allaah, ni kipi kinachokuliza?” Akasema: “Aliyoyafanya ´Imraan. al-Husayn ameingia akiwa ni mshirikina na hakuwahi kusimama wala kutazama upande wake. Wakati amesilimu ametimiza haki yake. Yamenigusa.”Wakati al-Husayn alipotaka kuondoka zake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Simama na umsindikize kwenye nyumba yake.”Alipotoka tu nje ya mlango wakamtukana na wakajitenga naye.”[1]

[1] Ibn Khuzaymah katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd”, uk. 120, al-Bayhaquy katika ”al-Asma’ was-Swifaat”, uk. 534, na adh-Dhahabiy katika ”al-´Uluww, uk. 24, aliyesema:

”´Imraan ni dhaifu.”

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithbaatu Swifat-il-´Uluww, uk. 75-77