1- Pindi mwenye busara atapomaliza kutengeneza undani wake anawajibika kutafuta elimu na kudumu juu ya hilo. Haiwezekani kufikia kitu katika ulimwengu huu kwa njia sahihi ya sawa isipokuwa kwa kuwa na ujuzi juu yacho. Haifai kwa aliye na akili kujitenga mbali kutokamana na kitu kinachopelekea Malaika kukunjua mbawa zao.

2- Haijuzu kwake katika kipindi cha jitihada kutafuta kujikurubisha kwa watawala au malengo ya kidunia. Ni ubaya uliyoje mwanachuoni kujidhalilisha kwa watu ambao hawana jengine isipokuwa kuyakimbilia mambo ya kidunia?

3- al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw amesema:

“Ni ubaya uliyoje mtu akaja nyumbani kwa mwanachuoni kumtafuta na akaja kupashwa khabari ya kwamba yuko kwa kiongozi au hakimu? Mwanachuoni na hakimu na kiongozi wapi kwa wapi? Mwanachuoni anatakiwa kuwa msikitini na kusoma Qur-aan.”

4- ash-Sha´biy amesema:

“Enyi wanafunzi! Msitafuta elimu kwa upumbavu na udadisi. Itafuteni kwa upole na utulivu.”

5- ash-Sha´biy amesema:

“Elimu hii haitafutwi isipokuwa na mtu aliye na sifa mbili; akili na ´ibaadah. Endapo atakuwa na akili lakini na asiwe na ´ibaadah, kutasemwa “Elimu hii haitafutwi isipokuwa tu na wale wenye kufanya ´ibaadah.” Matokeo yake ataacha kutafuta elimu. Na akiwa ni mwenye kufanya ´ibaadah na asiwe na busara, kutasemwa “Elimu hii haitafutwi isipokuwa na wale wenye akili.” Matokeo yake ataacha kutafuta elimu. Hii leo elimu hii inatafutwa na watu wasiokuwa na busara wala ´ibaadah vyote viwili.”

6- Sufyaan amesema:

“Elimu inaanza kwanza kwa kunyamaza, kisha kusikiliza, halafu kuhifadhi, kisha kuitendea kazi halafu kueneza.”

7- Abud-Dardaa amesema:

“Hauwi mwanachuoni mpaka pale utapojifunza na hauwi mwanachuoni mpaka pale utendee kazi yale uliyojifunza.”

8- Mwenye busara hajishughulishi na kutafuta elimu isipokuwa amekusudia kuitendea kazi. Anayetafuta elimu kwa malengo mengine basi itamzidishia tu kujifakhari na jeuri. Ukiongezea ya kwamba hatoitendea kazi vilevile. Madhara yanawapata zaidi wale wenye kumuiga kuliko yanavyompata yeye mwenyewe.

9- Maalik bin Diynaar amesema:

“Mtu akitafuta elimu kwa ajili ya kuitendea kazi, elimu yake humfurahisha. Akiitafuta kwa ajili ya malengo mengine, elimu yake humzidishia tu kiburi.”

10- Sufyaan ath-Thawriy amesema:

“Mwanachuoni ndio tabibu wa dini na pesa ndio ugonjwa wa dini. Ni lini mwanachuoni atawaponya wengine ikiwa yeye mwenyewe amejichukulia maradhi?”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 33-37
  • Imechapishwa: 12/11/2016