07. Baadhi ya waliokuja nyuma wanaivisha haki batili


Baadhi ya waliokuja nyuma wanasema kuwa hakuna tofauti yoyote kati ya mfumo wa Salaf na mfumo wa Mu´awwilah. Wanamaanisha kuwa mifumo yote miwili ni yenye kuafikiana juu ya kwamba Aayah na Hadiyth hazitolei dalili juu ya sifa za Allaah. Tofauti pekee ni kuwa Mu´awwilah wanaonelea kuwa kuna haja ya kuzifasiri na kuziteulia maana/makusudio yake. Kuhusiana na Salaf, waliacha kuziteulia maana kwa uwezekano wa kwamba maandiko yanaweza kuwa na maana nyengine.

Huu ni uongo wa wazi kwa Salaf. Hakuna yeyote katika wao aliyekanusha ile dalili yenye kuonyeshwa na sifa za Allaah inayolingana Naye Pekee. Bali maneno yao yanatoa dalili kuthibitisha sifa kwa jumla na kuwakemea wale wenye kuzikanusha au kumshabihisha Allaah na viumbe Wake. Kwa mfano amesema Nu´aym bin Hammad al-Kazaa´iy, ambaye ni mwalimu wa al-Bukhaariy:

“Yule mwenye kumshabihisha Allaah na viumbe Wake amekufuru. Mwenye kukanusha kitu katika yale Allaah amejisifia Mwenyewe amekufuru. Hata hivyo haizingatiwi kuwa ni kushabihisha kumthibitishia Allaah yale aliyojithibitishia Mwenyewe na yale ambayo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemthibitishia.”

Salaf wamezungumza sana kwa njia kama hiyo.

Kinachoonyesha kuwa Salaf walikuwa ni wenye kuthibitisha sifa na kwamba hawakuwa wakiafikiana kabisa na Mu´awwilah, ni kwamba Mu´awwilah walikuwa ni maadui zao. Walikuwa wakiwatuhumu kumshabihisha Allaah na viumbe na kumfanya kuwa na kiwiliwili kwa sababu tu wamethibitisha sifa. Lau kweli walikuwa wakiafikiana na Salaf kwamba maandiko hayatoi dalili juu ya sifa za Allaah, basi wasingelikuwa maadui zao au kuwatuhumu kwamba wanamshabihisha Allaah na viumbe na kumfanya kuwa na kiwiliwili. Hili ni jambo liko wazi kabisa na himdi zote ni za Allaah.