Ramadhaan ndio mwezi bora katika mwaka. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameufanya kuwa ni maalum swawm yake kuwa ni faradhi na nguzo ya nne katika nguzo za Uislamu. Amewawekea katika Shari´ah waislamu kusimama nyusiku zake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya vitano; kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji Nyumba.”[1]

“Atayesimama [nyusiku za] Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[2]

Allaah amemtunuku muislamu kukutana na Ramadhaan. Ndio maana anatakiwa kukimbilia kutumia fursa ya matendo mema na kujiepusha na maasi. Anatakiwa ajitahidi kutekeleza yale Allaah aliyomfaradhishia na khaswa swalah tano za faradhi. Ndio nguzo ya Uislamu na faradhi kubwa baada ya shahaadah. Hivyo ni wajibu kwa muislamu mwanaume na mwanamke kuihifadhi na kuiswali kwa wakati wake kwa unyenyekevu na utulivu.

Miongoni kwa wajibu mkubwa inapokuja kwa wanaume ni kuitekeleza swalah kwa mkusanyiko msikitini ambapo Allaah ameamrisha jina Lake litukuzwe na lidhukuriwe. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَارْكَعُوا مَعَ الرَّاكِعِينَ

“Simamisheni swalah na toeni zakaah na rukuuni pamoja na wanaorukuu.”[3]

حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ

“Shikamaneni na swalah na [khaswa khaswa] swalah ya katikati na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu.”[4]

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Kwa yakini wamefaulu Waumini. Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea.”

mpaka aliposema (´Azza wa Jall):

وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“… na wale ambao wanazihifadhi swalah zao. Hao ndio warithi, ambao watarithi al-Firdaws – wao humo ni wenye kudumu.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ahadi iliyopo baina yetu na wao ni swalah; hivyo basi yule atakayeiacha amekufuru.”[5]

´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Nimechunguza na kuona kuwa hakuna mwenye kuiacha isipokuwa ambaye ana unafiki unaojulikana.”[6]

Ee waja wa Allaah! Mcheni Allaah katika swalah zenu. Zihifadhini swalah zenu kwa mkusanyiko. Shaji´ishaneni nayo katika Ramadhaan na isiyokuwa Ramadhaan ili muweze kufuzu msamaha wa Allaah na thawabu tele na muepuke ghadhabu za Allaah, adhabu Yake na kujifananisha na maadui Wake wanafiki.

Baada ya swalah zakaah ndio faradhi ilio kubwa. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia yeye dini, wenye kupondoka kwenye haki na kuiacha batili, na wasimamishe swalah na watoe zakah – na hiyo ndio dini ilionyooka.”[7]

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Simamisheni swalah na toeni zakaah na mtiini Mtume ili mpate kurehemewa.”[8]

Zakaah ndio nguzo ya tatu na katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) imetajwa sambamba na swalah. Iadhimisheni kama Allaah alivyoiadhimisha na hakikisheni mmeitoa kwa Ikhlaasw kuwapa wenye kuistahiki pale ambapo ni wajibu. Itoeni kwa furaha na kwa kumshukuru mnemeeshaji (Subhaanah). Tambueni kuwa inakutakaseni na inatakasa mali zenu. Kwa njia hiyo mtakuwa mmemshukuru Ambaye amekuneemesheni na mmewaangalia ndugu zenu mafakiri. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

“Chukua katika mali zao swadaqah uwatwaharishe na uwatakase kwazo.”[9]

اعْمَلُوا آلَ دَاوُودَ شُكْرًا ۚ وَقَلِيلٌ مِّنْ عِبَادِيَ الشَّكُورُ

“Tendeni, enyi familia ya Daawuud, kwa shukurani!” Na ni wachache miongoni mwa waja Wangu wenye kushukuru.”[10]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) pindi alipomtuma Yemen:

“Hakika wewe unawaendea watu katika Ahl-ul-Kitaab. Walinganie washuhudie ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kuwa mimi ni Mtume wa Allaah. Wakikutii katika halo, wafunze kwamba Allaah amewafaradhishia kuswali swalah tano mchana na usiku. Wakikutii katika hilo, wafunze kuwa Allaah amewafaradhishia zakaah itayochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kupewa mafakiri wao. Wakikutii katika hilo, tahadhari na kuwachukulia mali zao nzurinzuri. Tahadhari na du´aa ya mwenye kudhulumiwa; kwani hakuna baina yake na baina ya Allaah kizuizi.”[11]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Katika mwezi huu muislamu anatakiwa kufanya bidii katika matumizi na kuwaangalia mafakiri na wale wenye kujizuia kuomba. Wawasaidie kufunga na kuswali swalah za usiku na kumuiga Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kutafuta radhi za Allaah (Subhaanah) na kushukuru neema Zake. Allaah amewaahidi wale wenye kujitolea kwa ajili Yake ujira mkubwa na malipo yasiyokuwa na kifani:

وَمَا تُقَدِّمُوا لِأَنفُسِكُم مِّنْ خَيْرٍ تَجِدُوهُ عِندَ اللَّـهِ هُوَ خَيْرًا وَأَعْظَمَ أَجْرًا

“Na chochote kile cha kheri mtakitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu, mtakikuta kwa Allaah. Ni bora na ujira mkubwa zaidi.”[12]

وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ

“Na chochote mtoacho katika kitu, basi Yeye Atakilipa. Naye ni mbora wa wenye kuruzuku.”[13]

Kitendo muhimu zaidi baada ya swalah na zakaah ni kufunga Ramadhaan ambayo ni moja katika nguzo za Uislamu zilizotajwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Uislamu umejengwa juu ya vitano; kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kwenda kuhiji Nyumba.”[14]

Ni wajibu kwa muislamu kuilinda swawm na kisimamo chake kutokamana na maneno na vitendo vyote ambavyo Allaah ameharamisha. Malengo ya swawm ni kumtii Allaah (Subhaanah), kuadhimisha makatazo Yake na kupambana na nafsi imtii Mola Wake na kuizoweza kujiepusha na yale Allaah aliyoharamisha.

Malengo yake sio kuacha tu chakula, kinywaji na vitu vyengine vinavyotengua swawm. Kwa ajili hii ndio maana imesihi kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swawm ni ngao. Mmoja wenu akifunga asiseme maneno ya upuuzi na wala asigombane. Mtu akimtukana aseme: “Nimefunga.”[15]

“Ambaye haachi uongo, kuutendea kazi na ujinga, Allaah hana haja kuacha chakula chake na kinywaji chake.”[16]

Tahadharini – Allaah akurehemuni – na yale yote yanayoidhuru swawm, kupunguza thawabu zake na kumkasirisha Mola (´Azza wa Jall) kama mfano wa ribaa, zinaa, kuiba, kuua kulikoharamishwa, kula mali ya mayatima na aina nyenginezo za dhuluma zinazohusiana na nafsi, mali na heshima, ghushi, khiyana, kuwaasi wazazi wawili, kukata udugu, chuki, kukatana kimakosa, kunywa pombe, madawa ya kulevya kama Qaat na sigara, kusengenya, uvumi, uongo, ushahidi wa uongo, madai batili, viapo vya uongo, kupunguza au kunyoa ndevu, kurefusha masharubu, kuwa na kiburi, nguo ya mwanaume yenye kuvuka kongo mbili za miguu, muziki, wanawake kutoka na nguo za mapambo, kutojisitiri kutokamana na wanaume na kujifananisha na wanawake wa makafiri inapokuja katika mavazi na kuvaa mavazi mafupi na mengine yote ambayo Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamekataza pamoja vilevile na filamu zisizofaa zilizo na yale Allaah aliyoharamisha kama uchi, nusu uchi, maneno mabaya na mambo mengine ya haramu yanayopatikana kwenye TV kama picha, muziki na propaganda batili.

Vilevile ni wajibu kwa kila muislamu, sawa awe amefunga au hakufunga, ajiepushe mbali na mambo yote ya kipuuzi kama karata na mengineyo. Huko kunashuhudiwa maovu na kunafanywa matendo ya maovu. Yanapelekea vilevile moyo kuwa msusuwavu na kugonjweka na kuchukulia usahali Shari´ah ya Allaah na yale Allaah aliyowajibisha kama swalah ya mkusanyiko na mambo mengine ya wajibu na yanapelekea vilevile mtu kutumbukia katika mambo mengi ya haramu.

Madhambi yote haya tuliyotaja ni haramu katika kila zama na pahala. Lakini hata hivyo ni haramu na khatari zaidi katika Ramadhaan kutokamana na utukufu na heshima yake.

Ee waislamu! Mcheni Allaah na jiepusheni na yale Allaah aliyokukatazeni na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtiini katika Ramadhaan na isiyokuwa Ramadhaan. Usianeni kuamrisha mema na kukataza maovu ili muweze kufuzu Pepo, furaha, utukufu na kuokoka duniani na Aakhirah.

Tunamuomba Allaah atukinge sisi, nyinyi na waislamu wengine wote kutokamana na yale yenye kusababisha ghadhabu Zake na atukubalie sote swawm na visimamo vyetu, awatengeneze watawala wa waislamu na ainusuru dini kupitia Wao na awakoseshe nusura maadui Wake kupitia wao na awawafikishe wote kuweza kuifahamu dini na kuwa na msimamo juu yake na kuhukumu na kuhukumiwa kwayo katika mambo yote. Hakika Yeye juu ya kila kitu ni muweza.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

[1] al-Bukhaariy (8) na Muslim (16).

[2] al-Bukhaariy (1901) na (2014) na Muslim (670).

[3] 02:43

[4] 02:238

[5] at-Tirmidhiy (2621), an-Nasaa’iy (463), Ibn Maajah (1079) na Ahmad (22987). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Ibn Maajah” (884).

[6] al-Bukhaariy (1496) na Muslim (19).

[7] 98:05

[8] 24:56

[9] 09:103

[10] 34:13

[11] al-Bukhaariy (1496) na Muslim (19).

[12] 73:20

[13] 34:39

[14] al-Bukhaariy (8) na Muslim (16).

[15] al-Bukhaariy (1904) na Muslim (1151).

[16] al-Bukhaariy (1903).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mufiyd fiy Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 27-30
  • Imechapishwa: 02/04/2022