06. Ulazima kwa kila muislamu kuitikia wito wa swalah kama anausikia

Swali 06: Nilikuwa mgeni kwa baadhi ya ndugu na swalah ya ´Aswr ikanikuta kwao. Nikawauliza kuhusu msikiti kama uko mbali au karibu wakanijibu kwamba uko mbali kidogo na wakasema bora ni kuswali mkusanyiko nyumbani. Lakini nikachelea pengine uko karibu na kwamba ningeweza kwenda msikitini. Lakini ndugu zangu wakagawanyika; wako ambao walitaka kwenda na mimi na wengine hawakutaka. Kwa hivyo nikaswali pamoja nao na wakanitanguliza mbele niwaswalishe. Kutokana na ufinyo wa chumba mmoja katika wao akaswali upande wangu wa kulia. Je, swalah yetu ni sahihi kwa sura kama hii? Ikiwa jibu ni “hapana”, je, nirudie swalah hiyo pekee au nirudie kila swalah niliyoiswali baada yake[1]?

Jibu: Swalah katika hali kama hii ni sahihi. Lakini ikiwa msikiti uko mbali kwa kiasi cha kwamba hawasikii adhaana hapana neno kuswali kwao sehemu yao. Lakini wakiwa wanasikia adhaana pasi na kipaza sauti basi itawalazimu kwenda msikitini. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote atakayesikia adhaana na asiitikie basi hana swalah isipokuwa akiwa na udhuru.”[2]

Ni wajibu kwa kila muislamu kuitikia wito ikiwa anausikia. Lakini akiwa si mwenye kuusikia isipokuwa kupitia spika basi haimlazimu kwenda msikitini. Endapo ataenda basi kitendo hicho ndio bora na chema zaidi.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/52-53)

[2] Ibn Maajah (785).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 24/11/2021