06. Tarawiyh


Ni jambo lisilokuwa na shaka kuwa Tarawiyh ni ´ibaadah kubwa iliyowekwa katika Shari´ah inayomkurubisha mwenye nayo kwa Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaswalisha waislamu nyusiku kadhaa. Pindi alipoanza kuchelea isije kufaradhishwa juu yao akaiacha na akawaambia badala yake waswali majumbani. Baada ya (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufariki na ukhaliyfah ukachukua ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) baada ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh), akaona namna ambavyo watu wametapakaa msikitini. Kulikuwa ambao wanaswali peke yao, wengine wanaswali wawiliwawili na wengine zaidi ya hapo. Ndipo akasema:

“Lau tutawakusanya nyuma ya imamu mmoja.”

Akafanya hivo. Akawakusanya wote nyuma ya Ubayy bin Ka´b. Akatumia dalili kitendo chake kwa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atayefunga Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Atayesimama [nyusiku za] Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[1]

Akatumia dalili vilevile kwa kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nyusiku zile. Akasema kwamba Wahy umekatika na kwa hiyo hakuna tena khatari ya kitendo hicho kuwa faradhi. Waislamu wakaswali mkusanyiko mmoja katika zama zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kadhalika katika zama za ´Umar na hali iliendelea kuwa hivo. Hadiyth zinashaji´isha katika hilo. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Atayesimama pamoja na imamu mpaka akamaliza ataandikiwa kama ameswali usiku mzima.”[2]

Ameipokea Imaam Ahmad na waandishi wa vitabu vya Sunan na mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh.

Ni dalili inayofahamisha kuwa imewekwa katika Shari´ah kuswali Tarawiyh mkusanyiko katika Ramadhaan na kwamba ni Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ya makhaliyfah wake waongofu. Waislamu kukusanyika wakati wa nyusiku hizi tukufu, kusikiliza Kitabu cha Allaah pamoja na kusikiliza mawaidha na makumbusho yanayoweza kutokea baadhi ya nyakati ni jambo lina manufaa makubwa.

Miongoni mwa hukumu zinazoweza kuwa zenye kufichikana kwa baadhi ya watu ni kule kudhania kuwa haifai Tarawiyh kuswaliwa chini ya Rakaa´ ishirini na wengine kufikiria kuwa haifai kuswaliwa zaidi ya Rakaa´ kumi na moja au kumi na tatu. Dhana zote hizi si za sawa. Bali ni za kimakosa na zinaenda kinyume na dalili. Dalili sahihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zinathibitisha kuwa swalah ya usiku inaweza kuswaliwa zaidi ya hivo. Hakuna kiwango maalum ambacho haifai kwenda kinyume nacho. Bali imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alikuwa anaweza kuswali Rakaa´ kumi na moja, Rakaa´ kumi na tatu na chini ya hapo katika Ramadhaan na isiyokuwa Ramadhaan.

Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa juu ya swalah ya usiku alisema:

“Swalah ya usiku ni mbili mbili. Iwapo mmoja wenu atachelea kuingia kwa asubuhi aswali Rakaa´ moja ambayo ni Witr kwa yale aliyoswali.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Hakuweka kiwango cha idadi maalum (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Ramadhaan wala isiyokuwa Ramadhaan. Kwa ajili hii ndio maana Maswahabah katika kipindi cha ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) walikuwa wanaweza kuswali Rakaa´ ishirini na tatu na wakati mwingine Rakaa´ kumi na moja. Yote haya yamethibiti kutoka kwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) na kwa Maswahabah katika zama zake.

Baadhi ya Salaf katika Ramadhaan walikuwa wanaswali Rakaa´ kumi na tatu na wakimaliza kwa Witr Rakaa´ tatu. Wengine walikuwa wakiswali Rakaa´ kumi na nne. Haya yametajwa na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) na wanachuoni wengine. Kadhalika ametaja kwamba suala hili ni pana na kwamba swalah inaweza kuswaliwa kwa njia mbalimbali. Amesema bora kwa ambaye atarefusha kisomo, Rukuu´ na Sujuud apunguze Rakaa´ na ambaye atakhafifisha kisomo, Rukuu´ na Sujuud azidishe idadi [ya Rakaa´]. Maneno ya Shaykh-ul-Islaam yana maana kama hii.

Anayetaka kuswali Rakaa´ ishirini na amalizie kwa Rakaa´ tatu za Witr ni sawa. Anayetaka kuswali Rakaa´ kumi na amalizie kwa Rakaa´ tatu za Witr ni sawa. Anayetaka kuswali Rakaa´ nane na amalizie kwa Rakaa´ tatu za Witr ni sawa. Hakuna neno iwapo mtu atapenda kuzidisha au kupunguza kuliko hivo. Hata hivyo lililo bora zaidi ni lile ambalo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya. Alikuwa akiswali Rakaa´ nane na akitoa Tasliym baada ya kila Rakaa´ mbili na akimalizia kwa Witr Rakaa´ tatu. Alikuwa akisoma kwa unyenyekevu, utulivu na kusoma Qur-aan kwa utungo. Imethibiti katika al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hazidishi, si katika Ramadhaan na isiyokuwa hiyo, Rakaa´ kumi na moja. Alikuwa akiswali nne [kwanza], usiulize juu ya uzuri na urefu wake. Kisha anaswali nne, usiulize juu ya uzuri na urefu wake. Halafu anaswali tatu.”[4]

Vilevile amepokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwake (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) usiku alikuwa akiswali Rakaa´ kumi na moja na akitoa Tasliym baada ya kila Rakaa´ mbili na akiwitiri kwa Rakaa´ moja[5].

Imethibiti pia kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati mwingine alikuwa akiswali swalah ya usiku Rakaa´ idadi ya chini ya hapo. Kadhalika imethibiti ya kwamba wakati mwingine alikuwa anaweza kuswali Rakaa´ kumi na tatu na akitoa Tasliym baada ya kila Rakaa´ mbili. Hadiyth hizi Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zinafahamisha kuwa swalah ya usiku inaweza kuswaliwa kwa njia mbalimbali na himdi zote zinamstahikia Allaah. Hakuna kiwango maalum ambacho hakijuzu isipokuwa hicho tu. Hii ni fadhila za Allaah, huruma na kuwawepesishia waja Wake na haya yanahusu Ramadhaan na isiyokuwa Ramadhaan.

Bora zaidi kwa ambaye anaswali nyuma ya imamu asitoke isipokuwa baada ya imamu kumaliza swalah yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayesimama pamoja na imamu mpaka akamaliza ataandikiwa kama ameswali usiku mzima.”[6]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Atayesimama pamoja na imamu mpaka akamaliza ataandikiwa kama ameswali usiku kutwa.”

Lililo bora kwa ambaye anaswali nyuma ya imamu ni yeye asiache swalah mpaka pale imamu atapomaliza swalah yake sawa ikiwa ataswali Rakaa´ kumi na moja, kumi na tatu, ishirini au idadi zisizokuwa hizo.

Katika swalah ya Tarawiyh na za faradhi ni wajibu kwa imamu kuzingatia hali za wale madhaifu katika mkusanyiko katika wazee na wengineo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule katika nyinyi atayewaongoza watu katika swalah basi akhafifishe. Katika wao kuna aliye dhaifu, mtumzima na mwenye haja.”[7]

Imamu anatakiwa kuwaangalia maamuma katika mkusanyiko na awe mpole kwao katika kisimamo cha Ramadhaan na katika yale masiku kumi ya mwisho. Watu hawako sawa. Wanatofautiana. Hivyo imamu anatakiwa kuangalia hali zao na kuwashaji´isha juu ya kuja na kuhudhuria. Akirefusha kupindukia atawatia uzito na kuwafanya wakimbie na wasihudhurie tena. Kwa hiyo anatakiwa kuwaji´isha kuhudhuria na kuwatia moyo kuja kuswali hata kama swalah itakuwa fupi. Swalah fupi ambayo watu wanapata kunyenyekea na utulivu ni bora kuliko swalah ambayo watu wanakosa unyenyekevu na badala yake wanachoshwa na kuhisi uvivu.

Itambulike kuwa kilichowekwa katika Shari´ah kwa muislamu katika kisimamo cha usiku sawa katika Ramadhaan na katika swalah zingine ni kuswali kwa unyenyekevu na utulivu katika hali ya kusimama, kukaa, kurukuu, kusujudu na usomaji wa Qur-aan. Asifanye haraka. Roho ya swalah itekelezwe kwa moyo na mazingatio. Inatakiwa kuswaliwa kama jinsi Allaah alivyoiamrisha kwa Ikhlaasw, ukweli, matumaini, woga na unyenyekevu. Allaah (Subhaanah) amesema:

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Kwa yakini wamefaulu waumini; ambao katika swalah zao huwa wananyenyekea.”[8]

 Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kipumbazo cha macho yangu kimefanywa katika swalah.”[9]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Unapotaka kuswali tawadha vilivyo. Kisha elekea Qiblah na useme “Allaahu Akbar”. Baada ya hapo soma kile kilichokuwia chepesi katika Qur-aan. Halafu rukuu mpaka upate utulivu hali ya kuwa umerukuu. Kisha inuka unyooke. Halafu sujudu mpaka upate utulivu hali ya kuwa umesujudu. Kisha kaa [kwenye sujudu] mpaka upate utulivu. Halafu sujudu mpaka upate utulivu hali ya kuwa umesujudu. Kisha ufanye hivo katika swalah yako yote.”[10]

Watu wengi wanaswali kisimamo cha Ramadhaan pasi na kuelewa kile wanachokisoma na bila ya kupata utulivu. Wanaswali kwa kudokoa. Hilo halijuzu. Ni dhambi. Swalah kwa njia hii haisihi. Utulivu ni nguzo katika swalah ambayo ni lazima ipatikane. Kama inavyofahamisha Hadiyth iliyotangulia punde tu. Ni wajibu kuhadhari na hilo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwizi mbaya kabisa ni yule anayeiba katika swalah yake.” Akaulizwa: “Ee Mtume wa Allaah! Ni vipi mtu ataiba katika swalah yake?” Akasema: “Hakamilishi Rukuu´ wala Sujuud yake.”[11]

Imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuamrisha mtu aliyedokoa swalah yake kuirudi.

Ee waislamu! Iadhimisheni swalah na itekelezeni kama alivyoiweka Allaah katika Shari´ah. Tumieni fursa ya mwezi huu mtukufu. Uadhimisheni – Allaah akurehemuni – kwa aina mbalimbali za ´ibaadah na sampuli za kujikurubisha kwa Allaah. Kimbilieni katika utiifu. Ramadhaan ni mwezi mtukufu ambao Allaah ameufanya kuwa ni uwanja kwa waja Wake. Ndani yake wanashindana juu ya utiifu na matendo ya kheri.

Jiepusheni na yale Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamekukatazeni. Mtiini katika Ramadhaan na isiyokuwa Ramadhaan. Usianeni kuamrishana mema na kukatazana maovu na linganieni katika mema ili muweze kufuzu Pepo, heshima, utukufu na kuokoka duniani na Aakhirah.

Tunamuomba Allaah atukinge sisi, nyinyi na waislamu wengine wote kutokamana na yale yenye kusababisha ghadhabu Zake na atukubalie sote swawm na visimamo vyetu, awatengeneze watawala wa waislamu na ainusuru dini kupitia Wao na awakoseshe nusura maadui Wake kupitia wao na awawafikishe wote kuweza kuifahamu dini na kuwa na msimamo juu yake na kuhukumu na kuhukumiwa kwayo katika mambo yote. Hakika Yeye juu ya kila kitu ni muweza.

Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah wake.

[1] al-Bukhaariy (1901) na (2014) na Muslim (760).

[2] at-Tirmidhiy (806) na an-Nasaa’iy (1605). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (447).

[3] al-Bukhaariy (991) na Muslim (749).

[4] al-Bukhaariy (1147) na Muslim (738).

[5] Muslim (736).

[6] at-Tirmidhiy (806) na an-Nasaa’iy (1605). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (447).

[7] al-Bukhaariy (90) na Muslim (466).

[8] 23:01-02

[9] an-Nasaa’iy (3939), Ahmad (12315) na wengine. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (3124).

[10] al-Bukhaariy (6251) na Muslim (397).

[11] Ahmad (11549), ad-Daarimiy (1328) na wengine. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (986).