06. Sifa ya tatu ya mwanamke ili aweze kuitengeneza jamii

Sifa ya tatu: Hekima.

Mwanamke anatakiwa awe na hekima katika kulingania katika dini ya Allaah na katika kuifikisha elimu kwa wale anaowazungumzisha. Hekima ni kukitia kitu mahala pake stahiki. Hivyo ndivyo walivyosema wanachuoni. Hii ni neema ya Allaah kwa mja kumtunuku hekima. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يُؤْتِي الْحِكْمَةَ مَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُؤْتَ الْحِكْمَةَ فَقَدْ أُوتِيَ خَيْرًا كَثِيرًا

“Humpa hekima amtakaye. Na yule anayepewa hekima, basi hakika amepewa kheri nyingi.”[1]

Mara nyingi malengo yanashindwa kufikiwa na kunatokea kasoro kunapokosekana hekima. Miongoni mwa hekima pindi mtu anapolingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall) ni kumteremsha yule mzungumzishwaji ngazi anayoistahiki. Akiwa ni mjinga anatakiwa kutaamiliwa namna inavyolingana na hali yake. Akiwa ni msomi lakini hata hivyo akawa na kitu katika uzembeaji, upuuzaji na ughafilikaji, anatakiwa kutaamiliwa namna inavyopelekea hali yake. Akiwa ni msomi lakini akawa na kitu katika kiburi na kuirudisha haki, atatakiwa kutaamiliwa namna inavyopelekea hali yake.

[1] 02:269

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dawr-ul-Mar´ah fiy Iswlaah-il-Mujtama´ https://www.sahab.net/home/?p=806
  • Imechapishwa: 02/02/2017