06. Sharti ya kukubaliwa kwa ulinganizi

Ikishathibiti kwamba kulingania kwa Allaah ni ´ibaadah, basi kama inavyotambulika ´ibaadah yoyote anayofanyiwa Allaah (Ta´ala) inakubalika kwa kutimia sharti mbili:

1 – Kumtakasia nia Allaah (Ta´ala).

2 – Iafikiane na alivofanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kitendo kilichotimiza sharti mbili hizi ndio kitendo chema ambacho Allaah (Ta´ala) amesema juu yake:

فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

”Hivyo yule anayetaraji kukutana na Mola wake basi na atende matendo mema na wala asimshirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote!”[1]

Kitendo kama hicho ndicho ambacho Allaah amesema juu yake:

بَلَى مَنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلّهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ فَلَهُ أَجْرُهُ عِندَ رَبِّهِ وَلاَ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ

“Sivyo hivyo! Yeyote anayeelekeza uso wake kwa Allaah naye ni mtenda mema, basi ana malipo yake kwa Mola Wake, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.”[2]

وَمَنْ أَحْسَنُ دِينًا مِّمَّنْ أَسْلَمَ وَجْهَهُ لِلَّـهِ وَهُوَ مُحْسِنٌ وَاتَّبَعَ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا

“Na nani aliye bora zaidi kwa dini kuliko yule aliyejisalimisha kwa Allaah ilihali ni mtendaji mema na akafuata mila ya Ibraahiym aliyejiengua na shirki na akaelemea Tawhiyd.”[3]

al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu maneno Yake Allaah (Ta´ala):

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا

“Ambaye ameumba kifo na uhai ili akujaribuni ni nani kati yenu mwenye matendo mazuri zaidi.”[4]

“Bi maana iliyotakasika na kupatiwa zaidi.” Wakasema: “Ee Abu ´Aliy! Nini maana ya iliyotakasika na kupatiwa zaidi?” Akajibu: “Kitendo kikiwa takasifu zaidi na kisiwe cha sawa hakikubaliwi, na kikiwa cha sawa na kisiwe takasifu zaidi hakikubaliwi. Ni lazima kiwe kimetakasika na kupatiwa zaidi.”

[1] 18:110

[2] 2:112

[3] 4:125

[4] 67:2

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas Aal ´Abdil-Kariym
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hujaj al-Qawiyyah ´alaa anna Wasaa-il-ad-Da´wah Tawqiyfiyyah, uk. 10
  • Imechapishwa: 29/07/2022