Allaah (Ta´ala) amesema:

 فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء رَبِّهِ

“Hivyo yule anayetaraji kukutana na Mola wake… “

Bi maana anakhofia na kuchelea. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Bi maana yule anayeamini kumuona Allaah siku ya Qiyaamah. Kwa sababu waumini watamuona Mola wao siku ya Qiyaamah na watafurahika kumuona zaidi kuliko watavyofurahika na neema zengine zote Peponi.”

Maneno ya Allaah (Ta´ala):

 فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

“… basi na atende matendo mema na wala asimshirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote!”

Yule asiyefanya matendo mema hawezi kumuona Mola wake. Kitendo hakiwi chema isipokuwa mpaka kitimize sharti mbili:

1- Kifanywe kwa kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall). Kitendo kisifanywe kwa ajili ya kujionyesha na kutaka kusikika. Kitendo kisalimike kutokamana na aina zote za shirki kubwa na ndogo.

2- Kitendo kiafikiane na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kisiwe na Bid´ah, mambo yaliyozuliwa na ukhurafi.

Kitendo kikikosa moja katika sharti hizi mbili basi hakiwi kitendo chema. Kinakuwa ni kitendo batili. Sharti ya kwanza ikikosekana, basi kitendo kinakuwa cha batili kutokana na ile shirki itakuwa imeingia ndani yake. Sharti ya pili ikikosekana, kinakuwa ni kitendo cha Bid´ah. Vilevile mambo yaliyozuliwa ni yenye kurudishwa na ni batili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu basi atarudishiwa mwenyewe.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo basi atarudishiwa mwenyewe.”[2]

Kwa hiyo kitendo hakiwi chema isipokuwa mpaka kitimize sharti hizi mbili. Amesema (Ta´ala):

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا

“Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi.”[3]

al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kwa utakaso wa nia na upatiaji.” Wakasema: “Ee Abu ´Aliy! Ni nini kwa utakaso wa nia na upatiaji?” Akasema: “Utakaso kifanywe kwa kumtakasia Allaah nia. Upatiaji kifanywe kwa kuafikiana na Sunnah za Mtume wa Allaah. Hakika kitendo kikiwa kimefanywa kwa ajili ya Allaah na kisiwe kwa upatiaji hakikubaliwi. Na kikiwa kimefanywa kwa upatiaji wa Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kisiwe kwa ajili ya Allaah hakikubaliwi. Kitendo kinachokubaliwi ni kile tu kilicho na utakaso na kwa upatiaji.”

[1] Muslim (1718).

[2] al-Bukhaariy (2697).

[3] 67:02

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 442-443
  • Imechapishwa: 26/08/2019