06. Mtume daima aliswali ´iyd katika uwanja wa kuswalia

Mahafidhi wahakiki wengi wametaja kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi sallam) siku zote alikuwa akiswali swalah ya ´Iyd sehemu ya uwanja[1]. Haya yanatiliwa nguvu na Hadiyth nyingi zilizipokelewa katika “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na “as-Swahiyh” ya Muslim, vitabu vya Sunan na vya Musnad kupitia njia nyingi kabisa. Hivyo haina budi kutaja baadhi yake katika haraka hii ili ipate kumbainikia msomaji muheshimiwa ya kuwa niliyoyasema ndio ya sawa.

1-  Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitoka siku ya Fitwr na siku ya Adhwhaa uwanjani[2]. Kitu cha kwanza alichokuwa akianza nacho ni swalah. Kisha akimaliza anawageukia watu waliokaa katika safu zao. Akiwapa mawaidha, kuwanasihi na kuwaamrisha. Ikiwa anataka kutuma kikosi, anafanya hivo[3], au kama akitaka kuamrisha kitu, basi anakiamrisha. Kisha anaondoka zake. Mpaka hii leo watu wanaendelea kufanya hivo.”[4]

2- ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Siku ya ´Iyd alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) asubuhi na mapema akienda uwanjani, akiwa na mkuki ameubeba mbele ya mikono yake. Anapofika kwenye uwanja anausimika chini mbele yake. Halafu akiswali na kuuelekea, hilo ni kwa sababu sehemu ya uwanja ilikuwa wazi na kwa ajili hiyo hakukuwa na kitu cha kukielekea.”[5]

3- al-Baraa´ bin ´Aazib amesema:

“Siku ya Adhwhaa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka kwenda Baqiy´[6] ambapo akaswali Rak´ah mbili. Kisha akatugeukia kwa uso wake na kusema: “Nusuuk yetu ya kwanza hii leo ni kuanza na swalah. Halafu tunarejea na kuchinja. Mwenye kufanya hivo, ameafikiana na Sunnah, na mwenye kuchinja kabla ya hapo, amefanya kitu alichoiharakishia familia yake na haina lolote haihusiani chochote na Nusuk.”[7]

4- Kulisemwa kuambiwa Ibn ´Abbaas:

“Je, ulishuhudia ´Iyd pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Akasema: “Ndio, lau ingekuwa sio kwa sababu ya udogo wangu nisingefanya hivo. Aliswali alipofika katika bendera ilio karibu na nyumba ya Kathiyr bin as-Swalt. Kisha akatoa Khutbah na baadaye akawaendea wanawake akiwa pamoja na Bilaal. Akawapa mawaidha, akawakumbusha na akawaamrisha kutoa swadaqah. Niliona namna wanavyorusha [swadaqah] kwa pupa kwenye kanzu ya Bilaal. Halafu akaenda yeye na Bilaal nyumbani kwake.”[8]

Muslim ameweka nyongeza katika upokezi wake kutoka kwa Ibn Jurayj:

“Nilimwambia ´Atwaa´: “Je, hii leo Imaam ana haki ya kuwaendea wanawake na kuwapa mawaidha?” Akasema: “Ninaapa ya kwamba wana haki ya kufanya hivo. Na ni kwa nini hawafanyi hivo?.”

[1] Tazama “Zaad-ul-Ma´aad” (01/172), “Fath-ul-Baariy” (02/361)  na “Mukhtaswar Zaad-il-Ma´aad”, uk. 44 ya Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab.

[2] Haafidhw amesema:

“Ni sehemu inayojulikana Madiynah iliyopo dhiraa elfumoja kutoka kwenye mlango wa msikiti.”

Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Ni uwanja wa kuswalia ambapo kunahifadhiwa mabegi ya mahujaji.”

Inaonekana kana kwamba sehemu hiyo iko upande wa mashariki ya msikiti wa Mtume karibu na makaburi ya al-Baqi´, kama inavyofahamisha Hadiyth ya tatu.

[3] Hapa kuna ishara yenye nguvu ya kwamba Khutbah ya ´Iyd haikukomeka tu na mawaidha na maelekezo, bali ni ukumbusho na maelekezo yote yanayopelekea katika manufaa ya Ummah.

[4] al-Bukhaariy (02/259-260), Muslim (03(20), an-Nasaa´iy (01/234), al-Muhaamiliy katika “Kitaab-ul-´Iydayn” (02/86), Abu Nu´aym katika “al-Mustakhraj” (02/10/02) na al-Bayhaqiy katika “as-Sunan” (03/280).

[5] al-Bukhaariy (01/354), Muslim (02/55), Abu Daawuud (01/109), an-Nasaa´iy (01/232), Ibn Maajah (01/392) na Ahmad (6286). Tamko hili ni la Ibn Maajah na ndio yametimia na mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh. Pia ameipokea al-Muhaamiliy (02/26-36), Abul-Qaasim ash-Shihaamiy katika “Tuhfat-ul-´Iyd” (14/16) na al-Bayhaqiy (03/284-285).

[6] Katika upokezi mwingine uwanjani.

[7] al-Bukhaariy (02/372) na tamko ni lake, Ahmad (04/282) na al-Muhaamiliy (02/90-96) na yale mapokezi mengine ni katika hizo mbili na mlolongo wa wapokezi wake ni mzuri.

[8] Ameipokea al-Bukhaariy (02/373) na tamko ni lake, Muslim (02/18-19), Ibn Abiy Shaybah (273/02), al-Muhaamiliy (38/39), al-Firyaabiy (85-93) na Abu Nu´aym katika “Mustakhraj” (02/08/2-9/01).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swalaat-ul-´Iydayn, uk. 15-19
  • Imechapishwa: 12/05/2020