06. Msingi wa pili: Kuwa na umoja katika dini na kujiepusha na kufarakana

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Msingi wa pili:

Allaah ameamrisha kuwa na umoja katika dini na akakataza kufarikiana kwayo. Allaah amebainisha haya ubainifu wenye kutosheleza ambao unafahamika na wajinga.

MAELEZO

Msingi huu unapatikana katika Qur-aan. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.” (03:103)

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ تَفَرَّقُوا وَاخْتَلَفُوا

“Na wala msiwe kama wale waliofarikiana na wakakhitilafiana” (03:105)

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ ۚ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّـهِ

“Hakika wale walioefarikisha dini yao na wakawa makundi makundi, huna lolote kuhusiana na wao. Hakika amri yao iko kwa Allaah.” (06:109)

شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ

“Amekuamuruni katika dini yale Aliyomuusia kwayo Nuuh na ambayo tumekuletea Wahy na tuliyomuusia kwayo Ibraahiym na Muusaa na ‘Iysaa kwamba: “Simamisheni dini na wala msifarikiane ndani yake”.” (42:13)

Haijuzu kwa waislamu kufarikiana katika dini yao. Badala yake wanatakiwa kuwa wamoja juu ya Tawhiyd:

إِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاعْبُدُونِ

“Hakika huu ummah wenu ni ummah mmoja; Nami ni Mola Wenu, hivyo basi niabuduni.” (21:92)

Haijuzu kwa Ummah wa Muhammad ukafarikiana katika ´Aqiydah, ´ibaadah na hukumu za dini yake. Mmoja anasema ni halali, mwingine anasema ni haramu pasi na dalili. Hili ni jambo halijuzu.

Kuwepo kwa tofauti ni kitu kisichokuwa na budi kwani ndio maumbile ya mwanaadamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا يَزَالُونَ مُخْتَلِفِينَ إِلَّا مَن رَّحِمَ رَبُّكَ

“Na wataendelea kukhitilafiana. Isipokuwa yule aliyemrehemu Mola Wako.” (11:118-119)

Lakini hata hivyo tofauti inatakiwa kutatuliwa kwa kurejeshwa katika Qur-aan na Sunnah. Mimi na wewe tukitofautiana basi ni wajibu kurejea katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ

“Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na siku ya Mwisho.” (04:59)

Ama kusema kila mmoja abaki katika madhehebu na ´Aqiydah yake na kwamba watu wako huru katika mitazamo yao na wanataka kuwepo uhuru katika ´Aqiydah na uhuru wa kuzungumza. Hii ndio batili ambayo Allaah amekataza. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Na shikamaneni kwa kamba ya Allaah nyote pamoja wala msifarikiane.” (03:103)

Wakati wa tofauti ni wajibu kwetu kuwa na umoja juu ya Kitabu cha Allaah. Hili linahusu hata masuala ya Fiqh pia. Tukitofautiana katika jambo basi tulirudishe katika dalili; yule ambaye atasapotiwa na dalili basi sisi tutakuwa naye, na atayekosea katika dalili basi sisi hatufuati kosa. Allaah (Jalla wa ´Alaa) hakutuacha tutofautiane na kufarikiana pasi na kutuwekea mizani yenye kubainisha kati ya yaliyo sahihi na kosa. Bali ametuwekea Qur-aan na Sunnah:

فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ

“Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah…”

yaani Qur-aan.

وَالرَّسُولِ

“… na Mtume…”

yaani Sunnah.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi nimekuachieni ambayo lau mtashikamana nayo barabara, basi hamtopotea baada yangu; Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu.”

Kwa kuwepo Sunnah ni kana kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yuko mbele yetu. Sunnah hizo zimeandikwa, zimesahihishwa na kuwekwa wazi. Hii ni katika fadhila za Allaah (Subhaanah wa Ta´ala) kwa ummah huu kutouacha bure. Badala yake ameuacha ukiwa na kitu chenye kuwaelekeza kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuwaelekeza katika usawa. Kuhusiana na mtu asiyetaka haki na anachotaka kila mtu abaki katika madhehebu na kundi lake na isitoshe anasema tuwe na umoja katika yale tunayokubaliana na tusameheane katika yale tunayotofautiana, haya bila ya shaka yoyote ni maneno ya batili.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 17-19
  • Imechapishwa: 18/05/2021