Baadhi yao walikemea yale aliyosimama kwayo Shaykh katika kusafisha na kutengeneza. Walisema kuwa hali za watu wa Najd zama za Shaykh ilikuwa nzuri na mitaa ilikuwa na wanachuoni na watu wenye uelewa. Kwa mujibu wao propaganda zilizotajwa kuhusu Da´wah ya Shaykh na kuzorota kwa hali kabla yake ni mambo yaliyozuliwa na wanahistoria. Maneno ya kipuuzi na makanusho kama haya ni yenye kutupiliwa mbali na hayahitajii nguvu nyingi. Vitabu vya wapinzani wake katika zama zake na vya wengineo kuhusiana na hilo vimejaa uongo na ulinganizi katika batili. Siwezi kufiria vyengine isipokuwa watu wenye elimu ya nchi za mashariki ndio walioko nyuma ya fikira hizi.

Akilini hakusihi kitu

ikiwa mchana unahitaji kuthibitishwa

Wako wengine waliosema kwamba Shaykh hazingatiwi kuwa ni Mujaddid kwa sababu alikuwa ni Hanbaliy mwenye kufuata kichwa mchunga. Ni kama kwamba ambaye alisema maneno haya anaona kuwa mtu hawezi kuwa Mujaddid mpaka atoke nje ya yale maoni ya madhehebu mane na maoni ya wanachuoni. Mtu kama huyu hajui ni nini maana ya kufanya upya na anaropokwa tu.

Kufanya upya ni kule kuondosha na kupiga vita mambo ya kikhurafi, shirki na Bid´ah  visivyokuwa na msingi wowote katika dini. Kufanya upya kunahusiana na kuibainisha dini ya haki na ´Aqiydah sahihi. Kama alivyofanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haikushurutishwa eti yule mwenye kufanya hivo atoke nje ya yale madhehebu mane na wanachuoni na badala yake alete uelewa mpya. Maimamu wakubwa katika Muhaddithuun walikuwa wakifuata madhehebu. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na Ibn-ul-Qayyim walikuwa ni Hanaabilah. Imamu an-Nawawiy na Ibn Hajar walikuwa ni Shaafi´iyyah. Imaam at-Twahaawiy alikuwa ni Hanafiy. Imaam Ibn ´Abdil-Barr alikuwa ni Maalikiy. Kufuata moja katika madhehebu haya mane haikuzingatiwa ni upotofu wala uchache wa elimu mpaka wafuasi wao watiwe hatiani. Kinyume chake yule mwenye kutoka nje ya maoni ya wanachuoni wenye kuzingatiwa ilihali si mwenye kustahiki kufanya hivo ndiye ambaye anahesabika kuwa ni mpotevu na mwenye kupondoka.

Shaykh (Rahimahu Allaah) hafuati maoni ya madhehebu yake kibubusa mpaka kwanza ayapimanishe na dalili. Yale yenye kuafikiana na dalili alikuwa ni mwenye kuyafuata, japokuwa maoni hayo hayako katika madhehebu yake. Kwa sababu lengo lake ilikuwa kufuata dalili. Jambo hili kwa dhati yake linazingatiwa ni kufanya upya katika Fiqh, tofauti na ufuataji wa kipofu na ushabiki wenye chuki.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 13-14
  • Imechapishwa: 22/07/2019