06. Matamshi ya baadhi ya waliokuja nyuma juu ya mfumo wa Salaf

Baadhi ya waliokuja nyuma wamesema kuwa mfumo wa Salaf katika sifa ni kuyapitisha maandiko vile kama yalivyotajwa pamoja na kuamini kwamba udhahiri wake sio makusudio yake. Maneno haya ambayo hayakufungamanishwa yanatakiwa kujadiliwa. Neno “udhahiri” limetajwa kwa jumla na hivyo linahitajia kupambanuliwa.

Ikiwa kunamaanishwa yale yenye kudhihiri kutoka katika maandiko yanayohusiana na sifa zinazolingana na Allaah bila ya kushabihisha, bila ya shaka hayo ndio makusudio/maana ya maandiko. Anayesema kinyume na akaamini hivo, ni mpotevu. Mwenye kuwanasibishia Salaf I´tiqaad hii ima amesema uongo au amekosea.

Ikiwa kunamaanishwa yale ambayo baadhi wanafikiria ya kwamba Allaah anafanana na viumbe Wake, bila ya shaka haya sio makusudio/maana ya maandiko. Isitoshe vilevile sio makusudio/maana ya maandiko kidhahiri. Ni jambo lisilowezekana katukatu Allaah akafanana na viumbe Wake na ni jambo lisilowezekana katukatu Qur-aan na Sunnah ikawa na kitu kisichowezekana kabisa. Mwenye kudhania ya kwamba haya ndio makusudio/maana ya udhahiri wake atambue kuwa amekosea. Udhahiri na maana yake ya wazi ni kuthibitisha sifa zinazolingana na Allaah pekee.

Kwa upambanuzi huu tutakuwa tumeyapata maandiko haki yake vile yanavyostahiki kimaandiko na kimaana.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 09/01/2020