06. Maana ya swawm


Swawm kilugha ni kujizuia. Ndio maana Malaika Jibriyl (´alayhis-Salaam) alisema kumwambia Maryam:

فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا ۖفَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا

“Basi kula na kunywa na litue jicho lako. Pindi utakapokutana na mtu yeyote [akikuuliza] mwambie: “Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa Rahmah ya kujizuia [na kusema], hivyo leo sitomsemesha mtu yeyote.”[1]

Imesemekena vilevile ya kwamba ni maneno ya ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Neno kujizuia (صَوْمًا) maana yake ni kujizuia na maneno. Swawm maana yake kilugha ni kujizuia na kitu chochote kile.

Swawm  maana yake Kishari´ah ni kujizuia na chakula, kinywaji na matamanio baina ya alfajiri ya pili mpaka kuzama kwa jua. Mwanzoni mwa Uislamu ilikuwa mtu anayekata swawm alikuwa anapata kula, kunywa na kufanya jimaa midhali hajalala. Akilala inakuwa haramu kwake kula, kunywa na kufanya jimaa. Waislamu walikuwa na hali hii kwa muda fulani. Kuna mtu alikuwa anaitwa Abu Salamah alikuwa akifanya kazi kwenye shamba lake mpaka ´Ishaa. Alipofika nyumbani akaomba chakula. Mke wake akaenda kumtengenezea chakula. Aliporudi akakuta amelala ambapo akamwambia kuwa chakula kimekuwa ni haramu kwake. Hivyo basi akaendelea kufunga na akaamka hali ya kuwa amefunga. Baada ya hapo akarudi kazini kwake na Dhuhr akaanguka na kuzimia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akapata khabari juu ya kuzimia kwake.

Mambo kama hayo yalimfika ´Umar bin al-Khattwaab na waumini wengine (Radhiya Allaahu ´anhum) waliokuwa karibu na wake zao. ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alichelewa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akaja nyumbani kwake ambapo akataka kufanya jimaa na mke wake. Mke wake akamjuza ya kwamba alilala. Akafikiri kuwa anatafuta nyudhuru na kuzua uongo ambapo akamwingilia kwa kumlazimisha. Alipomhakikishia kuwa kweli alilala akasikitika. Asubuhi akaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akamueleza kilichotokea. Ndipo Allaah (´Azza wa Jall) akateremsha:

أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إِلَىٰ نِسَائِكُمْ ۚ هُنَّ لِبَاسٌ لَّكُمْ وَأَنتُمْ لِبَاسٌ لَّهُنَّ ۗ عَلِمَ اللَّـهُ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَخْتَانُونَ أَنفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفَا عَنكُمْ ۖ فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Mmehalalishiwa usiku wa swawm kujamiiana na wake zenu; wao ni vazi kwenu na nyinyi ni vazi kwao. Allaah anajua kwamba nyinyi mlikuwa mkizihini nafsi zenu hivyo akapokea tawbah yenu na akakusameheni. Basi sasa changanyikeni nao [waingilieni] na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.” (02:187)

Neno “wa alfajiri” (مِنَ الْفَجْرِ) lilikuwa bado halijateremshwa. Ikapelekea baadhi ya Maswahabah, akiwemo ´Adiyy bin Haatim (Radhiya Allaahu ´anh), akachukua uzi mweupe na uzi mweusi na kuziweka chini ya mto. Wakaanza kula na kunywa mpaka kubainike weupe wa alfajiri katika weupe wa usiku na kujizuia baada ya hapo. Wakaja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia:

“Ee Mtume wa Allaah! Naweka nyuzi mbili chini ya mto wangu, uzi mweupe na uzi mweusi, ili niweze kubainikiwa na usiku na mchana.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Basi una mto mpana. Ni kuhusu weusi wa usiku na weupe wa mchana.” Ndipo Allaah (´Azza wa Jall) akateremsha:

مِنَ الْفَجْرِۖ

“… wa alfajiri… “[2]

Hapa ndipo ikabainika kuwa makusudio ya kamba nyeupe na nyeusi ni mwanga wa asubuhi na giza la usiku.

Kuanzia hapa tunapata kujua kuwa swawm inaanza kuanzia alfajiri ya pili mpaka jua linapozama. Makusudio ya alfajiri katika Aayah sio ile alfajiri ya kwanza. Kwa sababu alfajiri ya kwanza inatangulia takriban saa moja kabla ya kuingia alfajiri ya pili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Adhaana ya Bilaal na alfajiri ya uongo isikuzuieni na kula daku, isipokuwa alfajiri ya kweli… “[3]

Bi maana alfajiri ya sawa.

[1] 19:26

[2] al-Bukhaariy (4509) na Muslim (1090).

[3] Muslim (1094) na Ibn Maajah (706).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Istiqbaal Shahri Ramadhwaan, uk. 33-37
  • Imechapishwa: 09/06/2017