Imebainika kutokana na yale yaliyotangulia ya kwamba shahaadah maana yake ni hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah pekee. Yeye pekee ndiye mungu asiyekuwa na mshirika, kwa kuwa Yeye ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa. Neno hili tukufu limebeba ya kwamba waungu wote wanaoabudiwa sio wangu wa haki na kwamba ni wa batili. Hilo ni kwa kuwa hawastahiki kuabudiwa. Ndio maana mara nyingi kunaamrishwa kumwabudu Allaah na sambamba na hilo kunakanushwa kuabudiwa mwingine asiyekuwa Allaah. Kwa sababu kumuabudu Allaah hakusihi pamoja na kumshirikisha mwengine pamoja Naye. Amesema (Ta´ala):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote.” (04:36)

فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Basi atakayemkanusha twaaghuut [miungu ya uongo] na akamwamini Allaah, kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika. Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.” (02:256)

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na twaaghuut [miungu ya uongo].”” (16:36)

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayesema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` na akakufuru vinavyoabudiwa badala ya Allaah, imeharamika damu na mali yake.”[1]

Aidha kila Mtume alikuwa akiwaambia watu wake:

يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah – kwani hamna mungu mwingine wa haki asiyekuwa Yeye!” (07:59)

Kuna dalili zingine nyingi. Imaam Ibn Rajab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mja kuhakikisha na kuweka wazi maana hii ´hapana mungu isipokuwa Allaah` inapelekea ya kwamba asiwe na mungu mwengine asiyekuwa Allaah. Mungu ni yule anayetiiwa pasi na kuasiwa pamoja na kuadhimishwa na kutukuzwa na wakati huohuo apendwe, aogopwe, kutarajiwa, kutegemewa, kumuomba na kumuomba du´aa. Hayo yote hayasilihi kwa mwengine yeyote isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall).”[2]

Kwa ajili hii ndio maana pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaambia makafiri wa Qurayash waseme ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` walisema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu wote kuwa mungu mmoja? Hakika hili ni jambo la ajabu mno!” (38:05)

Walifahamu kuwa neno hili linabatilisha ´ibaadah zote za masanamu na kufanya ´ibaadah ni yenye kukomeka kwa Allaah pekee, jambo ambalo walikuwa hawataki. Kupitia haya imebainika ya kwamba maana ya shahaadah na pia inapelekea kumtakasia ´ibaadah Allaah na kuacha kuabudu visivyokuwa Yeye.

Mja akisema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` anakuwa ametangaza uwajibu wa kumpwekesha Allaah katika ´ibaadah na kubatilika kwa ´ibaadah za asiyekuwa Yeye kuanzia makaburi, mawalii, watu wema na vinginevyo. Haya yanabatilisha yale wanayoitakidi waabudia makaburi na watu mfano wao hii leo ya kwamba ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` maana yake ni kukubali kuwa Allaah yupo, kwamba Yeye ndiye Muumbaji, kwamba Yeye ndiye Muweza wa kuumba na mfano wa maana kama hizo. Kuna wengine wanasema kuwa maana yake ni hakuna Mwenye kuhukumu isipokuwa Allaah. Wanadhani kuwa yule mwenye kuamini hivo na akafasiri ´hapana mungu isipokuwa Allaah` hivo ameihakikisha Tawhiyd kabisa. Haijalishi kitu yale yote atayofanya katika kuabudu vyengine visivyokuwa Allaah na akawa na imani juu ya wafu na akajikurubisha kwao kwa kuwachinjia, kuwawekea nadhiri, kuyatufu makaburi yao na kutabaruku kwa udongo wao. Hawakutambua watu hawa kuwa makafiri wa mwanzo wameshirikiana nao katika imani hii na walikuwa wakitambua kuwa Allaah ndiye Muumbaji na Muweza wa kuumba. Walikuwa wakiyakubali hayo. Hawakuwaabudu wengine asiyekuwa Yeye isipokuwa kwa kudai kwao kwamba wanawakurubisha mbele ya Allaah. Haina maana kuwa walikuwa wakiitakidi kwamba wanaumba au wanaruzuku.

Kuhukumu ni sehemu ya maana ya ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`. Sio maana yake ya kikweli na inayotakikana. Kwa hivyo haitoshi kuhukumu kwa Shari´ah katika haki mbalimbali, adhabu za Kisharii´ah na katika magomvi muda wa kuwa bado kuna shirki katika ´ibaadah. Iwapo neno ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` maana yake ingelikuwa ni haya wanayodai watu hawa, basi kusingelikuwa kati ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na washirikina magomvi yoyote. Bali walikuwa wakikimbilia kumuitikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale anapowaambia wakubali kuwa Allaah ndiye Muweza wa kuumba, Allaah yupo au iwapo angeliwaambia wahukumu kwa Shari´ah katika umwagaji wa damu, mali na haki mbalimbali na wakati huohuo akawanyamazia ´ibaadah. Lakini watu hao walikuwa ni wafaswaha wa kiarabu walielewa endapo watatamka shahaadah basi watakuwa wamekubali kubatilika kwa ´ibaadah za masanamu na kwamba neno hili sio la kutamkwa peke yake lisilokuwa na maana yoyote. Kwa ajili hiyo ndio maana walilikimbia na wakasema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waungu wote kuwa mungu mmoja? Hakika hili ni jambo la ajabu mno!” (38:05)

Allaah amesema kuhusu wao:

إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ يَسْتَكْبِرُونَ وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ

“Hakika wao walipokuwa wakiambiwa: “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah”, hutakabari. Wanasema: “Je, sisi kweli tuache miungu yetu kwa ajili ya mshairi mwendawazimu?”” (37:35-36)

Walielewa kuwa ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` inapelekea kuacha kuabudu vyengine vyote asiyekuwa Allaah na wakati huohuo kumtakasia ´ibaadah Allaah pekee na kwamba iwapo wangeliyasema maneno hayo na wakaendelea kuyaabudu masanamu, basi wangelikuwa wamejigonga wao wenyewe. Kwa hiyo walikuwa wanakimbia kujigonga huku.

Waabudia makaburi leo hawakimbii kujigonga huku kunakotia aibu. Utawaona wanatamka shahaadah kisha wanaichengua kwa kuwaabudia wafu na kujikurubisha kwa makaburi kwa [kuwafanyia] aina mbalimbali za ´ibaadah. Khasara iliyoje kwa yule ambaye Abu Jahl na Abu Lahab walikuwa ni wajuzi zaidi wa shahaadah kuliko yeye!

Kwa kifupi ni kuwa yule atayelisema neno hili hali ya kuwa anatambua maana yake, akalitendea kazi kwa nje na kwa ndani yale inayopelekea katika kukanusha shirki na kuthibitisha ´ibaadah kwa Allaah pamoja na kuwa na imani yenye kukata kabisa kwa yale iliyobeba na kuifanyia kazi ndiye muislamu wa kweli. Yule atayelitamka, akalitendea kazi na yale inayopelekea pasi na kuamini maana yake ni mnafiki. Yule atayelitamka kwa ulimi wake, akatendea kazi kinyume chake shirki inayopingana nalo ni mshirikina mwenye kujigonga. Ni lazima vilevile pamoja na kutamka neno hili mtu atambue maana yake. Kwa kuwa hiyo ni njia inayopelekea kutendea kazi yale inayopelekea. Amesema (Ta´ala):

إِلَّا مَن شَهِدَ بِالْحَقِّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ

“… isipokuwa yule aliyeshuhudia kwa haki ilihali wanajua.” (43:86)

Kutendea kazi yale inayopelekea ni kule kumuabudu Allaah na kukanusha vile vyote vinavyoabudiwa badala ya Allaah, jambo ambalo ndio malengo ya neno hili.

Neno hili linapelekea vilevile kukubali Shari´ah mbalimbali za Allaah alizoweka katika ´ibaadah, mambo ya biashara, kuhalalisha, kuharamisha na kukataa Shari´ah zilizowekwa na wengine asiyekuwa Allaah. Amesema (Ta´ala):

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ

“Je, wanao washirika waliowaamuru dini yale ambayo Allaah hakuyaidhinisha?” (42:21)

Ni lazima kukubali Shari´ah za Allaah alizoweka katika ´ibaadah, mambo ya biashara na kuhukumu kwayo baina ya watu kwenye yale waliyotofautiana katika mambo ya kibinafsi na mengineyo. Sheria zilizotungwa na watu zinatakiwa kutupiliwa mbali. Hiyo ina maana vilevile ya kwamba inatakiwa kukataa Bid´ah na ukhurafi kwa sampuli zake zote ambayo yanazuliwa na kuenezwa na mashaytwaan wa kibinaadamu na wa kijini katika ´ibaadah. Atayekubali kitu katika hayo basi ni mshirikina, kama Alivyosema katika Aayah hii:

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ

“Je, wanao washirika waliowaamuru dini yale ambayo Allaah hakuyaidhinisha?” (42:21)

وَإِنْ أَطَعْتُمُوهُمْ إِنَّكُمْ لَمُشْرِكُونَ

“Mtakapowatii, basi hakika mtakuwa washirikina.” (06:121)

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ

“Wamewafanya marabi wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Allaah.” (09:31)

Imethibiti katika Hadiyth Swahiyh ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimsomea Aayah hii ´Adiyy bin Haatim at-Twaa-iy (Radhiya Allaahu ´anh) ambapo akawa amesema: “Ee Mtume wa Allaah! Hatukuwa tunawaabudu.” Akasema: “Je, hawakuwa wakikuhalalishieni alivyoharamisha Allaah na nyinyi mkavihalalisha na wakikuharamishieni alivyohalalisha Allaah na nyinyi mkaviharamisha?” Akajibu: “Ndio.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Basi huko ndio kuwaabudu.””[3]

Shaykh ´Abdur-Rahmaan bin Hasan (Rahimahu Allaah) amesema:

“Ikawa kule kuwatii kwao katika maasi ni kumuabudu asiyekuwa Allaah. Ndipo wakawafanya ni waungu wanaopingana na Tawhiyd ambayo ndio inafahamishwa na shahaadah… Ikapata kubaini ya kwamba neno la ikhlaasw limepingana na yote haya kutokana na vile linvyofahamisha neno hili.”[4]

[1] Muslim (23) na Ahmad (06/394).

[2] Kalimat-ul-Ikhlaasw, uk. 25.

[3] at-Tirmidhiy (3095).

[4] Fath-ul-Majiyd (02/653).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ma´naa laa ilaaha illa Allaah, uk. 20-27
  • Imechapishwa: 23/09/2023