06. Lulu kuhusu at-Twabaraaniy


6- at-Twabaraaniy (kfrk. 360) tabaka 11

adh-Dhahabiy ameandika wasifu wake katika “Tadhkirat-ul-Huffaadhw” na akasema:

”Haafidhw, Imaam, ´Allaamah na hoja Abul-Qaasim Sulaymaan bin Ahmad bin Ayyuub bin Mutwayr al-Lakhmiy ash-Shaamiy at-Twabaraaniy. Alizaliwa 260. Alianza kwenda katika masomo ya Hadiyth mwaka wa 273 na kisha baadaye huko Shaam, Makkah, al-Madiynah, Yemen, Misri, Baghdaad, Kuufah, Basrah, Aswbahaan, Jaziyrah na sehemu nyenginezo. Alipokea Hadiyth kutoka kwa zaidi ya waalimu 1000.

Alitunga kitabu “al-Mu´jam al-Kabiyr”. Kimepangwa kwa mujibu wa Maswahabah isipokuwa tu Abu Hurayrah. Ni kama kwamba amechukua zile Hadiyth za Abu Hurayrah akaziweka kipekee.

Kitabu chake “al-Mu´jam al-Awsatw” kina mijeledi sita mikubwa. Amekipanga kwa mpangilio wa waalimu zake. Ndani yake amepokea kutoka kwa kila mwalimu Hadiyth ya kushangaza. Kimefanana na “Kitaab-ul-Afraad” cha ad-Daaraqutwniy. Ndani yake ametaja ubora wa mwalimu wake na upana wa mapokezi yake. Alikuwa akisema kuwa kitabu hicho ndio roho yake. Amekiwekea bidii kubwa. Ndani yake kuna mazuri na mabaya yote.

Katika “al-Mu´jam as-Swaghiyr” ametaja Hadiyth zilizopokelewa na waalimu ambao kila mmoja amepokea Hadiyth moja tu.

Ametunga tungo nyingi. Alikuwa ni mmoja katika wanaume wa maudhui haya na alikuwa ni mkweli na mwaminifu.

at-Twabaraaniy alizaliwa mwaka wa 260 katika ´Akkaa. Mama yake anatokea ´Akkaa.

Abu Nu´aym amesema:

“at-Twabaraaniy alifika Aswbahaan mwaka wa 290. Alisikia Hadiyth kisha baadaye akasafiri. Halafu baadaye akarudi na akaishi huko miaka sitini.”

Ibn Marduuyah amesema:

“at-Twabaraaniy alifika mwaka wa 310. Abu ´Aliy bin Rustum al-´Aamil akampokea, akamkumbatia na akampa mshahara mpaka alipofariki.”

Abu ´Umar bin ´Abdil-Wahhaab as-Sulamiy amesema:

“Nilimsikia at-Twabaraaniy akisema: “Wakati Ibn Rustum aliporudi kutoka Persia alinipa dirhamu 500. Mwishoni mwa uhai wake akaanza kumzungumzia vibaya Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhmaa) ambapo nikamwacha na kamwe sikurudi kwake.”

Ibn Faaris, mtunzi wa “al-Lughah”, amesema:

“Nilimsikia Ibn-ul-´Aamid akisema: “Nilikuwa sidhani kama hapa duniani kuna jambo zuri kama uwaziri na utawala niliokuwemo mpaka pale nilipomwona at-Twabaraaniy akisoma Hadiyth pamoja na Abu Bakr al-Ja´abiy mbele yangu. at-Twabaraaniy akimshinda kwa hifadhi yake kali na al-Ja´abiy akimshinda kwa akili yake. Mpaka wakaanza kupandishiana sauti. al-Ja´abiy akasema: “Mimi nina Hadiyth ambayo hapa duniani hakuna isipokuwa kwangu tu.” at-Twabaraaniy akasema: “Ilete.” al-Ja´abiy akasema: ”Abu Khaliyfah ametuhadithia: Sulaymaan bin Ayyuub ametuhadithia …” at-Twabaraaniy akasema: ”Mimi ni Sulaymaan bin Ayyuub! Abu Khaliyfah ameisikia kutoka kwangu. Ipokee moja kwa moja kutoka kwangu…” al-Ja´abiy akaona haya. Nilitamani lau nisingelikuwa waziri na badala yake mimi ndiye nikawa at-Twabaraaniy na kufurahi kama alivyofurahi.”

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tadhkiyr-un-Naabihiyn, uk. 46-49
  • Imechapishwa: 11/06/2019