Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Suala la kwanza: Ujuzi, nao ni ujuzi wa kumjua Allaah, ujuzi wa kumjua Mtume Wake…

MAELEZO

Hii ndio elimu ya Kishari´ah inayotakikana kwa jamii na kwa mmojammoja. Ni kumjua Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa majina na sifa Zake, kuijua haki Yake juu yetu ambayo ni kumwabudu Yeye pekee asiyekuwa na mshirika. Kitu cha kwanza ambacho ni lazima kwa mja ni kumtambua Mola wake (´Azza wa Jall) na namna atakavyomwabudu.

Nao ni kumjua Allaah –  Atamjua vipi? Atamjua kwa alama Zake na viumbe Wake. Miongoni mwa alama Zake ni usiku na mchana. Miongoni mwa viumbe Vyake ni jua na mwezi. Yote hayo ubainifu wake unakuja – Allaah akitaka. Atamjua Allaah kwa alama Zake za kilimwengu na alama Zake za Qur-aan. Akisoma Qur-aan atamjua Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwamba Yeye ndiye kaumba mbingu na ardhi, kwamba Yeye ndiye kadhalilisha vyote vilivyomo mbinguni na ardhini, kwamba Yeye mwenye kuhuisha na kufisha, kwamba Yeye juu ya kila jambo ni muweza na kwamba Yeye ndiye Mwingi wa huruma Mwenye kurehemu. Yote haya yamo ndani ya Qur-aan yanayomtambulisha Allaah (´Azza wa Jall). Kwamba Yeye ndiye mwenye kutuneemesha kwa neema zoe na kwamba Yeye ndiye katuumba na katuruzuku. Ukiisoma Qur-aan utamjua Mola Wako (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa majina na sifa Zake na matendo Yake.

Ukitazama ulimwengu utamjua Mola Wako (Subhaanahu wa Ta´ala), kwamba Yeye ndiye kaumba viumbe hivi, kaudhalilisha ulimwengu huu na anauendesha kwa hekima na ujuzi Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Huku ndio kumjua Allaah (´Azza wa Jall).

Ujuzi wa kumjua Mtume Wake – Naye ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu yeye ndiye mwenye kufikisha kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Yeye ndiye muunganishi kati yetu sisi na Allaah (´Azza wa Jall) katika kufikisha ujumbe. Ni lazima umjue. Umjue ni nani, ujue nasabu yake, nchi yake, aliyokuja nayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ni vipi Wahy ulianza na ujue ni vipi alisimama kwa kuanza kulingania kwa Allaah (´Azza wa Jall) Makkah na al-Madiyanah. Unapaswa kujua historia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) japo kwa ufupi.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Muttwalib bin Haashim bin ´Abdil-Manaaf mpaka mwisho wa nasaba yake ya kinabii inayoishilia kwa Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vilevile unatakiwa kujua ni vipi aliishi kabla ya kutumilizwa, ni vipi alikuja kwa Wahy kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall) na alifanya nini (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kutimilizwa kwake. Utayajua hayo kwa kuisoma historia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haimstahikii kwa muislamu kutomjua Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni vipi utamfuata mtu ilihali humjui? Ni jambo lisiloingia akilini.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 20-22
  • Imechapishwa: 23/11/2020