Mwezi wa Ramadhaan unathibiti kuingia kwa kuona mwezi mwandamo kwa mtu kuuona mwenyewe, ukaonekana na mwengine au akaelezwa kuhusu hilo. Muislamu akishuhudia kuona mwezi mwandamo wa Ramadhaan basi kwa ushuhuda huu itathibiti kuingia kwa mwezi wa Ramadhaan. Amesema (Ta´ala):

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge.”[1]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa salalm):

“Mtakapouona basi fungeni.”[2]

Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza:

“Nilimpa khabari Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa salalm) kuhusu kuona mwezi mwandamo wa Ramadhaan ambapo yeye akafunga na akawaamrisha watu wafunge.”[3]

Usipoonekana mwezi au usionekane na muislamu yeyote ambaye ni mwadilifu basi italazimika kukamilisha idadi ya siku thelathini za Sha´baan. Hakuthibiti kuanza kwa mwezi kwa njia nyenginezo mbali na hizi mbili: kuona mwezi au kuikamilisha Sha´baan siku thelathini. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa salalm):

“Fungeni mtakapouona na fungueni mtakapouona. Ukifichikana kwenu basi kamilisheni idadi ya siku thelathini za Sha´baan.”[4]

Inathibiti kuisha kwa Ramadhaan kwa kuona mwezi mwandamo wa mwezi wa Shawwaal kwa ushahidi wa waislamu wawili ambao ni waadilifu. Wasipopatikana waislamu wawili wenye kutoa ushahidi basi ni lazima kukamilisha idadi ya siku thelathini za Ramadhaan.

[1] 02:185

[2] al-Bukhaariy (1900) na Muslim (1080).

[3] Abu Daawuud (2342) na al-Haakim katika ”al-Mustadrak” (01/423) ambaye ameisahihisha.

[4] al-Bukhaariy (1909) na Muslim (1081).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 152-153
  • Imechapishwa: 14/04/2020