06. Kuritadi kwa maneno


1- Kuritadi kwa maneno: Ni kwa mfano mtu akatamka kwa matamshi ya kufuru na ya shirki pasi na kulazimishwa. Ni mamoja akawa anakusudia kweli, anafanya mzaha au anacheza. Akitamka maneno ya kufuru anahukumiwa kuritadi. Isipokuwa ikiwa tu ametenzwa nguvu. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ

”Wamekwishasema neno la kufuru na wakakufuru baada ya Uislamu wao.”(at-Tawbah 09:74)

Amesema (Ta´ala) juu ya wale waliosema:

“Hatujapata kuona watu kama wasomaji wetu hawa; ndimi zao zinasema uongo sana, matumbo yao yanapenda kula sana na ni waoga wakati wa mapambano – yaani wanamkusudia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake.”

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ ۚ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Ukiwauliza, basi bila shaka watasema: “Hakika sisi tulikuwa tunaporoja na tunacheza.” Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?”  Msitoe udhuru; mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (at-Tawbah 09:65-66)

Wamekufuru baada ya kuamini kwao. Kwa sababu tu walisema:

“Hatujapata kuona watu kama wasomaji wetu hawa; ndimi zao zinasema uongo sana, matumbo yao yanapenda kula sana na ni waoga wakati wa mapambano – yaani wanamkusudia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake.”

Walipojua kuwa Allaah amemteremshia Wahy Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu maneno yao, ndipo wakaja kutoa udhuru na huku wakisema:

إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ

”Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza.”

na kwamba wanaongea ili kupunguza uchovu wa safari. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumjali kabisa na akawa hazidishi neno isipokuwa kusema:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?”  Msitoe udhuru; mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.”[1]

Ni dalili inayofahamisha kwamba yule mwenye kutamka matamshi ya kufuru bila ya kulazimishwa basi anaritadi. Haijalishi kitu hata kama atadai ya kwamba anafanya mzaha na kucheza. Hapa kuna Radd kwa Murji-ah wa leo ambao wanaonelea kuwa mtu haritadi akizungumza maneno ya kufuru mpaka ayaamini moyoni mwake yale yaliyosemwa na ulimi wake.

Hali kadhalika yule anayeomba badala ya Allaah, akataka msaada badala ya Allaah na akasema: “Ewe fulani! nisaidie!”, “Ewe fulani! Niokoe!”, ambapo akawa anawaomba wafu na walio ndani ya makaburi, akawaomba mashetani na majini, akawaomba viumbe walioko mbali na yeye na akawataka msaada. Akiomba badala ya Allaah na akataka uokozi badala ya Allaah kutoka kwa wafu na viumbe walioko mbali na yeye anakufuru kwa kufanya hivo. Huku ndio kukufuru kwa maneno. Isipokuwa tu yule aliyelazimishwa. Allaah (Subhaanah) amesema:

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِين

”Atakayemkufuru Allaah baada ya kuamini kwake [atachukuliwa hatua] – isipokuwa yule aliyelazimishwa na huku moyo wake ukawa umetua juu ya imani. Lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao watapata ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kubwa. Hivyo kwa sababu wao wamefadhilisha maisha ya dunia kuliko ya Aakhirah na kwamba Allaah hawaongoi watu makafiri.”(an-Nahl 16:106)

لَّا يَتَّخِذِ الْمُؤْمِنُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِ الْمُؤْمِنِينَۖ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَلَيْسَ مِنَ اللَّـهِ فِي شَيْءٍ إِلَّا أَن تَتَّقُوا مِنْهُمْ تُقَاةً

”Waumini hawawachukui makafiri kuwa wapenzi wao badala ya waumini na yule atakayefanya hivyo, basi hatokuwa na chochote mbele ya Allaah. Isipokuwa mkiwa mnajilinda kwayo na shari zao.” (Aal ´Imraan 03: 28)

Huyu ndiye ambaye katenzwa nguvu.

Kwa hivyo mtu akitamka neno la kufuru, kwa njia ya kwamba ima akalazimishwa atamke na vinginevyo anauawa au kuadhibiwa, hakune neno akatamka neno kwa kiasi kile alicholazimishwa na wakati huohuo moyo wake uwe umetua juu ya imani. Atamke kwa ulimi wake tu. Kuhusu moyo hakuna yeyote awezaye kuuendesha isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) pekee.

إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ

“… isipokuwa yule aliyelazimishwa na huku moyo wake ukawa umetua juu ya imani.”

Aayah hii iliteremka kuhusu ´Ammaar bin Yaasir (Radhiya Allaahu ´anh). Washirikina walikuwa wanamuadhibu na wanamlazimisha kumtukana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akatamka maneno ambayo ndani yake kuna kumtukana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lengo lake ilikuwa kujinasua kutoka kwa makafiri. Wakati huohuo ndani ya moyo wake hapakuwepo bughudhi yoyote kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala kuchukia dini ya Uislamu. Bali moyo wake ulikuwa umetua juu ya imani. Aliposema maneno haya akaja hali ya kuwa ni mwenye kujuta kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza yaliyotokea. Akamuuliza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Vipi unahisi moyoni mwako?” Akajibu: “Wenye kutua juu ya imani.” Ndipo akamwambia: “Wakirudi na wewe rudi.”[2]

[1] Tamko la kisa hiki kimepokelewa Ibn Abiy Haatim (10046), Ibn Jariyr katika “Tafsiyr yake” (10/195-196). Ameipokea kwa njia ya Mawsuulah na Mursalah zinazopeana nguvu.

[2] Ameipokea Ibn Jariyr katika “Tafsiyr yake (14/216), Ibn Abiy Haatim katika “ad-Durar al-Manthuur” (05/170-171) na Haafidhw Ibn Hajar katika “al-Fath al-Baariy” (12/327).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 20-22
  • Imechapishwa: 03/05/2018