13- Atapofikwa na alama za kufa, basi ni juu ya yule aliye karibu naye afanye yafuatayo:

1- Amtamkishe shahaadah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Watamkisheni maiti wenu ´Laa ilaaha illa Allaah`.[Yule ambaye maneno yake ya mwisho wakati wa kufa yatakuwa ni ´Laa ilaaha illa Allaah` ataingia Peponi, hata kama atalitamka mata moja tu maishani mwake, hata kama kabla ya hapo alifanya aliyoyafanya.”]

Alikuwa akisema:

“Mwenye kufa ilihali anajua ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah ataingia Peponi.”

Katika Hadiyth nyingine imekuja:

“Mwenye kufa hali ya kuwa hamshirikishi na Allaah chochote, ataingia Peponi.”

Amezipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake, nyongeza katika ile Hadiyth ya kwanza inapatikana kwa Ibn Hibbaan (719) na al-Bazzaar.

2 na 3 – Amuombee du´aa na asiseme maneno yoyote ispokuwa ya kheri. Kutokana na Hadiyth ya Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) aliyesimulia kwamba: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtakapokuwepo kwa mgonjwa au kwa maiti, basi semeni yaliyo ya kheri. Kwani Malaika wanaitikia “Aamiyn” kwa yale mnayoyasema.”

Ameipokea Muslim, al-Bayhaqiy (03/384) na wengineo.

14- Kumtamkisha shahaadah anayetaka kukata roho sio kule kumtamkia nayo mbele yake na kumsikilizisha nayo. Bali inatakiwa kumwamrisha kuitamka. Hilo ni tofauti na wanavyodhania baadhi ya watu. Dalil ya hilo ni Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kwamba:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtembelea mtu mmoja katika Answaar ambapo akamwambia: “Ee khaali au mjomba wangu! Sema “Laa ilaaha illa Allaah”. Akasema: “Je, ni kheri kwangu nikisema “Laa ilaaha illa Allaah?” Akamjibu: “Ndio.”

Ameipokea Imaam Ahmad (03/152, 154, 268) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh juu ya masharti ya Muslim.

Husayn al-Hanafiy amesema:

15- Kuhusu kumsomea Suurah “Yaa Siyn” na kumwelekeza upande wa Qiblah hakukusihi dalili juu ya hayo. Bali ni jambo alilichukia Sa´iyd bin Musayyib kuelekezwa huko na akasema: “Je, maiti huyu si mtu muislamu?”

Zur´ah bin ´Abdir-Rahmaan ameeleza kwamba alishuhudia wakati Sa´iyd bin Musayyib alipokuwa kwenye maradhi na hapo kwake alikuwepo Salamah bin ´Abdir-Rahmaan mara Sa´iyd akazimia. Abu Salamah akaamrisha kitanda chake kielekezwe Ka´bah. Baadaye Sa´iyd alipozinduka akasema: “Mmekigeuza kitanda changu?” Wakasema: “Ndio.” Akamtazama Abu Salamah ambapo akasema: “Wamefanya hivo kwa utambuzi wako?” Akasema: “Mimi ndiye nimewaamrisha.” Ndipo Sa´iyd kaamrisha kirudishwe kitanda chake kama kilivyokuwa.”

Ameipokea Ibn Abiy Shaybah katika “al-Muswannaf” (04/76) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Zur´ah.

16- Hapana ubaya muislamu akahudhuria kukata roho kwa kafiri ili kumlingania katika Uislamu kwa matarajio akasilimu. Hilo ni kutokana na Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh):

“Kijana mmoja wa kiyahudi ambaye alikuwa akimtumikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliuguwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaenda kumtembelea. Akakaa karibu na kichwa chake na kumwambia: “Silimu!” ambapo mtoto yule akamtazama baba yake na akamwambia: “Mtii Abul-Qaasim (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)!” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akatoka nje na usema: “Sifa zote njema anastahiki Allaah ambaye amemwokoa kutokamana na Moto.” [Alipokufa akawaambia: “Mswalieni mwenzenu.”].

Ameipokea  al-Bukhaariy, al-Haakim, al-Bayhaqiy na Ahmad (03/175, 227, 280, 260) na nyongeza ni yake katika upokezi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 09-11
  • Imechapishwa: 19/12/2019