06. Kuingia ndani zaidi katika kuitikia wito wa Allaah


Lengo la sita: Kuingia ndani katika kuitikia wito wa Allaah

Miongoni mwa malengo kuu ya hajj ni kuingia ndani zaidi katika kuitikia wito wa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala), kutekeleza maamrisho Yake, kumtii na kujisalimisha na Shari´ah Yake. Haya ni malengo makubwa katika malengo ya hajj. Inatakikana kuzindukana nayo. Haya yanapata kudhihiri katika mambo na nyanja mbalimbali katika hajj. Miongoni mwa mambo na nyanja hizo muhimu zaidi ni Talbiyah wanazokariri mahujaji mara mamia na zaidi ya hapo kwa mujibu wa uchangamfu wa hali ya kila mmoja. Katika Talbiyah neno “Labayk” linakariri mara nne. Ni neno la kuitikia. Kwa msemo mwingine ni kama vile mtu anasema “Mimi nimekuitikia Wewe, ee Allaah, nimenyenyekea ma nimejisalimisha na amri na Shari´ah Yako. Umeniita kuja kuhiji Nyumba Yako ambapo nikasema “Nimekuitikia Wewe, ee Allaah, nimekuitikia Wewe.” Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَأَذِّن فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالًا وَعَلَىٰ كُلِّ ضَامِرٍ يَأْتِينَ مِن كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍ

“Tangaza kwa watu hajj watakufikia kwa kutembea kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda watakuja kutoka katika kila njia pana za milima zilioko mbali kabisa.”[1]

Matokeo yake watu wa imani wakaja na majibu wakimuitikia Mwingi wa rehema hali ya kusema:

“Tumekuitikia Wewe, ee Allaah, tumekuitikia Wewe.”

Bi maana sisi ni wenye kukuitikia Wewe, ee Allaah, wenye kujisalimisha na maamrisho Yako na wenye kunyenyekea yale Uliyotuitia. Kukariri kwa neno “Labayk” ni kwa ajili ya kusisitiza kule kuitika. Pale unaposema:

“Nimekuitikia Wewe, ee Allaah, nimekuitikia Wewe.”

maana yake nimekubali ukweli wa kukubali, nimenyenyekea ukweli wa kunyenyekea, nimejisalimisha ukweli wa kujisalimisha.

Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa yule mwenye kufanya Talbiyah kunyanyua sauti yake katika Talbiyah hiyo. Imekuja katika Hadiyth kutoka kwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Jibriyl amenijia mimi na akasema: “Ee Muhammad! Waamrishe Maswahabah zako wazinyanyue sauti zao kwa ajili ya Talbiyah. Kwani ni katika nembo za hajj”[2]

Imekuja vilevile kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba aliulizwa: “Hajj ni ipi?” Akasema: “al-´Ajj” wath-Thajj”.[3]

al-´Ajj ni kunyanyua sauti wakati wa kuleta Talbiyah.

Kunyanyua sauti kwa Talbiyah ni jambo lina maana kubwa na athari tukufu kwa mja juu ya kuhakikisha Kwake kuitikia na kujisalimisha na maamrisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Imekuja katika Hadiyth iliopokelewa na at-Tirmidhiy kutoka kwa Sahl (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna muislamu yeyote anayeleta Talbiyah isipokuwa huleta Talbiyah ambaye yuko kuumeni kwake au kushotoni kwake katika mawe, miti au udongo mpaka ikatike ardhi upande wa kulia na wa kushoto.”[4]

Pale unapoleta Talbiyah na kunyanyua sauti yako kwa Talbiyah hiyo, basi mawe, miti na milima, kuliani kwako na kushotoni kwako, vinaleta Talbiyah kwa Talbiyah yako. Sisi mahuhaji, ijapokuwa hatusikii Talbiyah ya mawe, miti na milima, lakini hata hivyo tuko na yakini juu ya hayo. Kwani ambaye ametukhabarisha juu ya hayo ni yule mkweli mno na mwenye kusadikishwa ambaye hazungumzi kwa matamanio yake – swalah na salaam zimwendee yeye. Miongoni mwa ushahidi juu ya hayo katika Qur-aan ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ ۗ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا

“Zinamsabihi mbingu saba na ardhi na vilivyomo ndani yake; hakuna kitu chochote isipokuwa kinamtukuza kwa himdi Zake, lakini hamzielewi tasbihi zao. Hakika Yeye ni mvumilivu, Mwingi wa kusamehe.”[5]

يَا جِبَالُ أَوِّبِي مَعَهُ وَالطَّيْر

”Ee milima! Rejesheni kumtukuza [Allaah] pamoja naye na ndege pia.”[6]

Talbiyah hii ambayo inakariri kukariri kwa wingi kupitia midomoni mwa mahujaji sio kukariri ambako hakuna maana yoyote na kurudirudi ambako hakuna faida yoyote nyuma yake. Hapana sivyo hivyo. Bali kukariri huku ni kwa ajili kuingie zaidi ndani ya moyo wako kumuitikia Allaah (´Azza wa Jall) na kutekeleza kwako maamrisho Yake. Isiwe tu Makkah na katika kwenda kwako huku na kule katika nembo za hajj. Bali iwe hivo katika maisha yako yote. Allaah amekuita uje kufanya hajj ambapo ukasema “Nimekuitikia, ee Allaah, nimekuitikia”. Ewe ambaye Allaah amekuamrisha kufanya hajj ambapo ukaitikia wito ukaja ukikusudia Nyumba ya Allaah ya kale hali ya kuwa ni mwenye kutaraji rehema Zake na kuogopa adhabu Zake, ni upi msimamo wako kunako maamrisho mengine yaliyobaki? Ni upi msimamo wako juu ya swalah ambayo ndio nguzo ya dini na ndio nguzo kuu baada ya shahaadah mbili? Ni upi msimamo wako juu ya swawm? Ni upi msimamo wako juu ya zakaah? Ni upi msimamo wako katika kujitenga mbali na makatazo na kuachana na makatazo? Ikiwa wewe ni mwenye kuyatekeleza basi mshukuru Allaah na umuombe akuzidishie. Na ikiwa ni mwenye kuzembea na mwenye kuyapoteza, basi ihesabu nafsi yako kabla hujafanyiwa hesabu siku ya Tulioahidiwa.

Umeitwa katika swalah ambayo ndio muhimu na kubwa zaidi kuliko hajj. Umeitwa katika swawm ambayo ndio ndio muhimu na kubwa zaidi kuliko hajj. Umeitwa katika faradhi zengine kwa jumla na kujiepusha na ya haramu – ni upi msimako wako, ewe mwenye kuleta Talbiyah, ewe mwenye kukariri neno la ´Talbiyah` katika Nyumba ya Allaah na katika kwenda kwako huku na kule kati ya nguzo pamoja na maamrisho ya Allaah na faradhi za Uislamu? Hivi kweli inamstahikia muislamu kunyanyua sauti yake kwa Talbiyah katika hajj kisha anapoitwa katika swalah haitikii wito? Anapoitwa katika kufunga haitikii wito? Anapoitwa ili kujitenga mbali na mambo ya haramu na madhambi haitikii wito?

Kwa ajili hii tunatakiwa kuhisi ya kwamba Talbiyah na matendo mengine ya hajj yanafanya kuingia kwa undani zaidi katika kule kumuitikia Allaah na kujisalimisha na maamrisho Yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Wangapi katika watu ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewakirimu wakafaidika na hajj zao na wakarudi katika miji yao wakiwa na hali bora zaidi hali ya kuwa ni wenye kuchunga maamrisho, kujiepusha mbali na makatazo, kuhakikisha uchaji Allaah (´Azza wa Jall). Kwa ajili hii imekuja katikati ya Aayah ya hajj maneno Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَتَزَوَّدُوا فَإِنَّ خَيْرَ الزَّادِ التَّقْوَىٰ

“Chukueni masurufu. Hakika bora ya masurufu ni kumcha Allaah.”[7]

[1] 22:27

[2] Ahmad (21678) na wengineo.

[3] Ibn Maajah katika ”Sunan” yake (2896).

[4] at-Tirmidhiy katika ”Jaami´ah” (828).

[5] 17:44

[6] 34:10

[7] 02:197

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 28-35
  • Imechapishwa: 18/08/2018