Vivyo hivyo inahusiana na kuamini Vitabu. Ni wajibu kuamini kwa jumla ya kwamba Allaah (Subhaanah) amewateremshia Vitabu Manabii na Mitume Yake kwa ajili ya kubainisha haki na kulingania katika dini Yake. Amesema (Ta´ala):

لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ

“Hakika Tuliwatuma Mitume Wetu kwa hoja bayana na tukateremsha pamoja nao Kitabu na mizani ili watu wasimamie kwa uadilifu.” (57:25)

كَانَ النَّاسُ أُمَّةً وَاحِدَةً فَبَعَثَ اللَّـهُ النَّبِيِّينَ مُبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ وَأَنزَلَ مَعَهُمُ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِيَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ فِيمَا اخْتَلَفُوا فِيهِ

“Watu walikuwa ummah mmoja kisha Allaah akawatuma Mitume wabashiriaji na waonyaji na akateremsha pamoja nao Kitabu kwa haki ili kihukumu baina ya watu katika waliyokhitilafiana kwayo.” (02:213)

Vilevile inatupasa kuamini kwa njia ya upambanuzi vile ambavyo Allaah amevitaja. Mfano wa hivyo ni Tawraat, Injiyl, az-Zabuur na Qur-aan. Qur-aan ndio bora zaidi, ndio ya mwisho, ndio yenye kuvihukumu na ndio yenye kuvisadikisha. Ni wajibu kwa watu wote kuiamini, kuifuata na kuhukumu kwacho pamoja na zile Sunnah zilizosihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa kuwa Allaah (Subhaanah) amemtuma Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hali ya kuwa ni Mtume kwa majini na wanaadamu na vilevile akamteremshia Qur-aan hii ili aweze kuhukumu kwayo na akaifanya kuwa ni ponyo kwa yale yaliyomo kifuani na yenye kubainisha kila kitu na ni mwongozo na rehema kwa waumini. Amesema (Ta´ala):

وَهَـٰذَا كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ مُبَارَكٌ فَاتَّبِعُوهُ وَاتَّقُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Kitabu hiki Tumekiteremsha kilichobarikiwa, hivyo basi kifuateni na cheni mpate kurehemewa.” (06:155)

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ

“Tumekuteremshia Kitabu chenye kubainisha kila kitu na ni mwongozo na rehema na bishara kwa waislamu.” (16:89)

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖ فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الْأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ

“Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote; Yeye ambaye pekee anao ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, anayehuisha na kufisha. Basi mwaminini Allaah na Mtume Wake, Nabii asiyejua kuandika wala kusoma, ambaye anamwamini Allaah na maneno Yake – mfuateni ili mpate kuongoka.” (07:158)

Kuna Aayah nyingi zilizo na maana kama hii.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah as-Swahiyhah wa maa yudhwaadduhaa, uk. 08-9
  • Imechapishwa: 30/05/2023