06. Hawa ndio maswahiba zako katika njia uliyoichukua

Allaah (Jalla wa ´Alaa) ametufaradhishia katika kila swalah kusoma Suurah “al-Faatihah”. Mwisho wake imekuja:

اهدِنَــــا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ

“Tuongoe Njia iliyonyooka.” (01:06)

Njia hiyo ndio njia ya Allaah (Jalla wa ´Alaa):

وَأَنَّ هَـذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا

“Hii ndio Njia yangu iliyonyooka.” (06:153)

Maneno Yake (Ta´ala):

اهدِنَــــا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ

“Tuongoe njia iliyonyooka.”

Bi maana tuongoze, utuelekeze na ututhibitishie katika Njia iliyonyooka.

صِرَاطَ الَّذِينَ أَنعَمتَ عَلَيهِمْ

“Njia ya uliowaneemesha.” (01:07)

Ni kina nani wanaopita katika Njia hii? Ni wale ambao Allaah amewaneemesha katika Manabii, wakweli, mashahidi na watu wema – ni uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao! Hawa ndio wenzako unaopita nao katika Njia hii:

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَأُوْلَـئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَـئِكَ رَفِيقًا

“Na wenye kumtii Allaah na Mtume, hao wako pamoja na wale aliowaneemesha Allaah miongoni mwa Manabii, na wakweli, na mashahidi na Watu wema – na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!” (04:69)

Kwa hivyo usibabaike na wewe uko katika Njia hii. Wenzako na viongozi wake ni watu bora zaidi. Usibabaike hata kama njia za vichochoro zimekuwa nyingi, mapote yamekuwa mengi, wapinzani wamekuwa wengi, usiwajali. Kwa kuwa wewe unafuata jambo la kihakika: Njia ya Allaah (´Azza wa Jall).

غَيرِ المَغضُوبِ عَلَيهِمْ وَلاَ الضَّالِّينَ

“Siyo ya waliokasirikiwa wala waliopotea.” (01:07)

Bi maana sio Njia ya waliokasirikiwa wala waliopotea. Waliokasirikiwa ni wale walio na elimu na hawakuifanyia kazi, kama mfano wa mayahudi. Ni watu wana elimu lakini hata hivyo hawakuifanyia kazi. Elimu kama mwenye nayo haikufanyia kazi inakuwa ni hoja dhidi yake siku ya Qiyaamah. Elimu ikiwa ni maneno tu bila ya vitendo itampeleka mwenye nayo Motoni. Ni yapatikane matendo. Kuwa na elimu bila ya matendo ni kama mti usiyoleta na matunda. Una faida gani mti huyu usiokuwa na matunda? Hivyo ndio maana Allaah amewakasirikia. Ni watu wako na elimu na hawakuifanyia kazi. Wamestahiki ghadhabu za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hata kama wataona wao ndio watu bora, walio mbele na ni watu wa maendeleo. Wamo upotofuni. Wamo katika khasira za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

غَيرِ المَغضُوبِ عَلَيهِمْ وَلاَ الضَّالِّينَ

“Siyo ya waliokasirikiwa wala waliopotea.”(01:07)

Bi maana sio njia ya waliopotea. Hawa ni wale wenye kufanya matendo; wanamuabudu Allaah, wanajitahidi na kuipa nyongo dunia, lakini wanafanya yote haya pasi na elimu na uongofu kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Matendo yao ni bure hayatowafaa kitu. Wao wamepotea katika Njia, wamepotea katika Njia iliyonyooka. Matendo wanayofanya ni kujichosha bila ya faida yoyote. Miongoni mwa watu hawa ni pamoja vilevile na manaswara. Ni watu wanaofanya ´ibaadah, utawa na mengineyo, lakini wanafanya yote haya pasina elimu. Wamepotea. Wako katika makosa. Kinachozingatiwa sio juhudi na bidii anazofanya mtu pasi na kuisibu haki.

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com