06. Hadiyth “Mwenye kusahau ambapo akala au kunywa basi akamilishe swawm yake… “

Hadiyth ya sita

6- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kusahau ambapo akala au kunywa basi akamilishe swawm yake. Kwani si vyengine Allaah ndiye kamilisha na kumnywisha.”

Maana ya kijumla:

Shari´ah hii imejengwa juu ya wepesi na urahisi na makalifisho kwa kiasi cha uwezo wa mtu na mtu kutokuchukuliwa kwa yale yanayotoka nje ya uwezo na khiyari yake. Miongoni mwa hayo ni kwamba yule mwenye kula au kunywa au akafanya kitu kingine kinachofunguza mchana wa Ramadhaan au mchana wa swawm nyingine, basi aendelee na swawm yake. Swawm yake ni sahihi.  Kwa sababu hakufanya kwa kupenda kwake mwenyewe. Hilo si jengine isipokuwa limetokamana na Allaah ambaye kamlisha na kumnywesha.

Kutofautiana kwa wanachuoni:

Wanachuoni wengi wanaonelea kuwa kula na kunywa kwa kusahau hakuharibu swawm ya mtu. Wametofautiana juu ya jimaa kama ina hukumu moja kama ya kula na  kunywa na kwamba haiharibu swawm? Imaam Ahmad anaonelea kuwa jimaa inaharibu swawm ijapokuwa atakayefanya hivo ni mjinga au mwenye kusahau. Endapo atafanya hivo mchana wa Ramadhaan basi kunawajibisha kutoa kafara. Ni miongoni mwa mambo ambayo amepwekeka nayo Ahmad. Dalili ya hilo ni uelewa wa Hadiyth ambapo umekomeka katika kula na kunywa pasi na jimaa. Ni dalili inayoonyesha kuwa ni mambo mawili tofauti. Jengine ni kwamba kufanya jimaa kwa kusahau ni jambo gumu kufikiriwa tofauti na kula na kunywa.

Maimamu wengine akiwemo Abu Haniyfah, ash-Shaafi´iy, Abu Daawuud, Ibn Taymiyyah na wengineo wameonelea kuwa hakuharibu swawm. Wametoa dalili kwa haya yafuatayo:

1- Kutokana na yale aliyopokea al-Haakim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh):

“Mwenye kula katika Ramadhaan kwa kusahau basi halazimiki kulipa wala kutoa kafara.”

Ibn Hajar, na ni sahihi, amesema:

“Jambo la kula limeenea katika jimaa na mengineyo.”

2- Ujumla uliyopokelewa katika mfano maneno Yake (Ta´ala):

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie tukisahau au tukikosea.” (02:286)

 “Ummah wangu umesamehewa makosa, kusahau na yale waliyotenzwa nguvu.”

3- Wale ambao wanaonelea kinyuma juu ya kusihi kwa swawm yake nao pia wamekubali kwamba hapati dhambi. Akiwa ni mwenye kupewa udhuru basi udhuru ni wenye kuenea. Hakuna sababu yoyote ya kuyatofautisha [hayo mawili].

Faida zinazochukuliwa kutoka katika Hadiyth:

1- Kusihi kwa swawm ya ambaye amekula, amekunywa au amefanya jimaa kwa kusahau.

2- Hapati dhambi kwa kule kula au kunywa. Kwa sababu hakufanya kwa kutaka kwake mwenyewe.

3- Maana ya:

“Kwani si vyengine Allaah ndiye kamilisha na kumnywisha.”

ni kwamba hakufanya hivo kwa kutaka kwake mwenyewe. Allaah ndiye kamkadiria hivo kusahau ndani ya swawm yake.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-´Allaam Sharh ´Umdat-il-Ahkaam, uk. (01/319-321)
  • Imechapishwa: 25/05/2018