06. Hadiyth “Mtume wa Allaah alikuwa akibusu hali ya kuwa amefunga… “

Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

681- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuunganisha swawm ambapo bwana mmoja katika waislamu akasema: “Hakika wewe unafunga kwa kuunganisha, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Ni nani katika yenu ambaye ni mfano wangu? Mimi hulala nikilishwa na kunyweshwa na Mola wangu.” Walipokataa kuacha kuunganisha swawm akaunganisha kufunga siku mbili mfululizo kisha wakaona mwezi mwandamo ambapo akasema: “Lau mwezi mwandamo ungelichelewa basi ningekuzidishieni.” Bi maana kwa njia ya kuwakaripia kwa vile walikataa kukoma kuunganisha.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

682- Amepokea tena (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyeacha maneno ya uongo, kuyatendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Abu Daawuud na tamko ni lake.

683- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akibusu hali ya kuwa amefunga na akichanganyikana ilihali amefunga, lakini alikuwa ni mwenye kuweza kujizuia vyema kuliko nyinyi.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim na tamko ni lake. Katika upokezi mwingine amezidisha:

“… katika Ramadhaan.”[4]

MAELEZO

Inafaa kwa mfungaji kumbusu mke wake, kuchanganyikana naye, akamkumbatia na mfano wa hayo? Ndio, inafaa kwake kufanya hivo kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiyafanya hayo. Lakini ikiwa anachelea juu ya nafsi yake kuharibika kwa swawm yake na anaogopa endapo atambusu au kumkumbatia mke wake basi atatokwa na manii, basi haitojuzu. Ama akiwa anawezi kuimiliki nafsi yake basi tunacho sisi kiigizo chema kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (1965) na Muslim (1103).

[2] al-Bukhaariy (1903) na Abu Daawuud (2362).

[3] al-Bukhaariy (1927) na Muslim (1106).

[4] Muslim (1106).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mukhtaswar ´alaa Buluugh-il-Maraam (2/410-414)
  • Imechapishwa: 24/04/2020