Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ama faradhi zake ni sita:

1- Kuosha uso kukiwemo vilevile kusukutua na kupalizia. Mpaka wa uso ni pale nywele za kichwa zinapoanzia mpaka kwenye kidevu, na kuanzia kwenye sikio la kulia mpaka la kushoto.

2- Kuosha mikono miwili mpaka kwenye visugudi.

3- Kupangusa kichwa chote kukiwemo masikio.

4- Kuosha miguu miwili mpaka kwenye vifundo vya miguu.

5- Kuyafanya kwa kupangilia.

6- Muwaalaah [kiungo kimoja kisiwahi kukauka kabla ya kuoshwa cha kufuatia].

Dalili ya hilo ni Kauli Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلاةِ فاغْسِلُواْ وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُواْ بِرُؤُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَينِ

“Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya swalah, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visugudi na panguseni vichwa vyenu na miguu yenu hadi vifundoni.”[1]

Dalili ya kupangilia ni Hadiyth:

Dalili ya kupangilia ni Hadiyth:

“Anza kwa Alichoanza nacho Allaah.”[2]

Na dalili ya Muwaalaah ni Hadiyth ya mtu aliyeacha sehemu bila ya kuosha. Imepokelewa kwamba wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliona mtu aliyeacha sehemu katika mguu wake kiasi cha dirhamu hakikufikiwa na maji, hivyo akamuamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kurudia na kutia [wudhuu´] upya[3].

MAELEZO

Faradhi za wudhuu´ ni sita. Uso unatakiwa kuoshwa kukiwemo vilevile kusukutua na kupalizia, mikono inatakiwa kuoshwa mpaka kwenye visugudi, kichwa chote kinatakiwa kupanguswa kukiwemo masikio, miguu miwili inatakiwa kuoshwa mpaka kwenye vifundo vya miguu, vinatakiwa kuoshwa kwa mpangilio na kiungo kimoja kisiwahi kukauka kabla ya kingine. Faradhi hizi za wudhuu´ ni kwa mujibu wa maneno ya Allaah (Jalla wa ´Alaa):

Kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amevitaja kwa mpangilio basi ni wajibu kuviosha kwa mpangilio:

“Anza kwa Alichoanza nacho Allaah.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitawadha kama alivyobainisha Allaah. Kwa hiyo ni wajibu kwetu kutawadha kama alivyotawadha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Faradhi ya sita ni kwamba kiungo kimoja kisiwahi kukauka kabla ya kuoshwa cha kufuatia. Mtu anatakiwa kutawadha wudhuu´ wa papo kwa hapo na asiache muda ukarepa. Aoshe viungo vyote kabla ya kukauka. Dalili ya hilo ni kwamba wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomuona mtu mmoja kwenye unyayo wake kuna mahali kiasi cha sarafu haikupatwa na maji akamwamrisha kutawadha na kuswali tena upya. Ni dalili inayoonyesha ya kwamba jambo la kufuatanisha na kuwahi kuosha kiungo kimoja kabla ya kingine kukauka ni la wajibu. Hakumwambia mtu yule kuosha tu sehemu ile ambayo haikupatwa na maji; bali alimwamrisha kurudi kutawadha na kuswali tena upya. Kwa hiyo ni lazima kufuatatanisha na kuwahi kuosha kiungo kimoja kabla ya kingine kukauka. Kwa hiyo kwa mfano mtu ataosha viungo vyake vya mwili vyote na akauchelewesha mguu wake wa kushoto mpaka ukawa umekauka, basi ni wajibu kurudi kutawadha tena upya. Kwa sababu hakufuatanisha.

[1] 05:06

[2] an-Nasaa’iy (2962). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Tamaam-ul-Minnah”, uk. 88.

[3]Abu Daawuud (175) na Ahmad (15595). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (168).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumtaaz, uk. 66-67
  • Imechapishwa: 25/06/2018