06. Baadhi ya maovu yanayofanyika maulidini


Isitoshe, sherehe hizi za mazazi – licha ya kwamba ni Bid´ah – mara nyingi hazisalimiki na maovu mengi kukiwemo kuchanganyika wanawake na wanamme, kutumia nyimbo na ala za muziki, kunywa kilevi na madawa ya kulevya na maovu mengine. Pengine yakatokea ambayo ni makubwa zaidi kuliko hayo ambayo ni ile shirki kubwa. Hayo yanapatikana kwa kuchupa mpaka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au mawalii wengine, kumwomba du´aa, kumtaka uokozi wa haraka, kuonelea kuwa anajua yaliyofichikana na mengineyo katika mambo ya kikafiri yanayofanywa na watu wengi pindi wanaposherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wengineo wanaowaita kuwa ni mawalii. Imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Tahadharini na kuchupa mpaka katika dini. Hakika kilichowaangamiza waliokuwa kabla yenu ni kuchupa mpaka katika dini.”[1]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Msinisifu kwa kupindukia kama manaswara walivomsifu kwa kupindukia ´Iysaa mwana wa Maryam. Hakika mimi si venginevyo ni mja. Hivyo semeni mja na Mtume wake.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh).

[1] Ibn Maajah (3029) na an-Nasaa´iy (3057).

[2] al-Bukhaariy (3261).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr minal-Bid´ah, uk. 10-12
  • Imechapishwa: 12/01/2022