Aina muhimu zaidi ni Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah kwa sababu ndio ambayo walilingania kwayo Mitume. Vitabu vikateremshwa kwa ajili yake. Kwa ajili yake kukawekwa Jihaad katika njia ya Allaah. Lengo ni Allaah aabudiwe pekee na kuachwe kuabudiwa waungu wengine.

Hakuna viumbe wanaopinga Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah wala Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametaja Aayah nyingi juu ya hilo. Ametaja kwamba makafiri wanakubali kwamba Allaah ndiye Muumbaji na Mwenye kuruzuku anayehuisha na kufisha na anayeendesha mambo. Hakuna na kipingamizi juu ya haya. Lakini kuamini aina hiyo haimfanyi mtu akawa ni muislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita watu ambao wanakubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Alihalalisha damu na mali zao. Lau Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ingelikuwa ni yenye kutosha basi Mtume asingeliwapiga vita. Wala kusingelikuwa na haja ya kuwatumiliza Mitume. Ni dalili inayofahamisha kwamba yenye kutakikana na muhimu zaidi ni Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Ama kuhusu Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah ni dalili ya Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na yenye kuelekeza huko. Kwa ajili hiyo utaona pindi Allaah anapoamrisha kuabudiwa basi hutaja kwamba Yeye ndiye ambaye kaumba mbingu na ardhi na ndiye Mwenye kuendesha viumbe Wake ili kuithibitisha Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na kuwafanya makafiri kumwabudu Allaah pekee. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaamrisha waseme kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, wakasema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya waabudiwa kuwa ni mungu Mmoja?  Hakika hili ni jambo la ajabu mno!”[1]

وَإِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَحْدَهُ اشْمَأَزَّتْ قُلُوبُ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ ۖ وَإِذَا ذُكِرَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ إِذَا هُمْ يَسْتَبْشِرُونَ

“Anapotajwa Allaah pekee, basi nyoyo za wale wasioamini Aakhirah hunyweya kwa ghadhabu na kukengeuka na wanapotajwa wengineo pasi Naye, tahamaki wanafurahikia.”[2]

إِنَّهُمْ كَانُوا إِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ يَسْتَكْبِرُونَ وَيَقُولُونَ أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ

“Hakika wao walipokuwa wakiambiwa ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah` hufanya kiburi na wanasema: “Je, hivi kweli sisi tuache waabudiwa wetu kwa ajili ya mshairi mwendawazimu?”[3]

Wao hawaitaki Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Walikuwa wanataka kuwepo kwa waungu wengi na kila moja aabudu anachotaka.

[1] 38:05
[2] 39:45
[3] 37:35-36

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 29-31
  • Imechapishwa: 04/06/2019