Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya uombezi ni maneno Yake (Ta´ala):

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Na wanaabudu asiyekuwa Allaah ambao [hawawezi] kuwadhuru na wala kuwanufaisha na wanasema: “Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.” (10:18)

Kuna aina mbili za uombezi:

1 – Uombezi wenye kukanushwa.

2 – Uombezi wenye kuthibitishwa.

Uombezi wenye kukanushwa ni ule wenye kutafutwa kutoka kwa asiyekuwa Allaah katika yale yasiyoweza kufanya yeyote isipokuwa Allaah. Dalili ni maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِمَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ ۗ وَالْكَافِرُونَ هُمُ الظَّالِمُونَ

“Enyi mlioamini! Toeni sehemu katika vile Tulivyokuruzukuni kabla haijafika siku ambayo hakutakuweko mapatano [ya fidiya] humo wala urafiki wala uombezi na makafiri wao ndio madhalimu.” (02:254)

Uombezi wenye kuthibitishwa ni ule wenye kutafutwa kutoka kwa Allaah na mwombezi amekirimiwa uombezi na muombewaji ni yule ambaye Allaah ameridhia maneno yake na vitendo vyake baada ya kupewa idhini. Amesema (Ta´ala):

مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ

“Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake?” (02:255)

MAELEZO

Kuna aina mbili ya uombezi:

Aina ya kwanza ya uombezi ni ule ambao Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameukanusha na ni ule uombezi unaokuwa pasi na idhini Yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakuna yeyote awezaye kushufaia mbele ya Allaah isipokuwa kwa idhini Yake. Pindi kiumbe bora kabisa na Mtume wa mwisho Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atapotaka kuwaombea watu siku ya Qiyaamah, basi ataanguka hali ya kusujudu mbele ya Mola Wake, amuombe, amtape na kumsifu mpaka pale atapoambiwa:

“Nyanyua kichwa chako, zungumza utasikizwa, omba utapewa.”[1]

Hatoombea isipokuwa baada ya idhini Yake.

Aina ya pili ya uombezi wenye kuthibitishwa ni ule unaokuwa kwa wale wenye kumwabudu Allaah peke yake. Mshirikina hautomfaa kitu uombezi wa waombezi. Yule mwenye kuyachinjia na kuyawekea nadhiri makaburi ni mshirikina na hautomfaa kitu uombezi.

Kwa kufupisha ni kwamba uombezi wenye kukanushwa ni ule wenye kutafutwa pasi na idhini ya Allaah au kuombewa mshirikina. Ama kuhusu uombezi wenye kuthibitishwa ni ule unaokuwa baada ya idhini ya Allaah na unakuwa kwa wale wenye kumwabudu Allaah peke yake.

[1] al-Bukhaariy (7510) na Muslim (193).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 21-22
  • Imechapishwa: 18/08/2022