Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Katika hayo kunaingia pia kumchinjia asiyekuwa Allaah, kama ambaye anamchinjia jini au kaburi.”

MAELEZO

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amepiga mfano kwa kusema:

“… kama ambaye anamchinjia jini au kaburi.”

Kuchinja ni ´ibaadah. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ

“Sema: “Hakika swalah yangu na kichinjwa changu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu, hana mshirika.”[1]

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

“Basi swali kwa ajili ya Mola wako na chinja kwa ajili Yake.”[2]

Endapo mtu atamchinjiia asiyekuwa Allaah basi atahesabika amemfanyia ´ibaadah asiyekuwa Allaah. Kwa hiyo anakuwa mshirikina. Mtunzi amepigia mfano hilo na kusema kama kuchinjia kwa ajili ya jini. Mtu akilichinjia jini au akamchinjia aliyemo ndani ya kaburi amefanya shirki. Kadhalika akilichinjia kaburi, nyota au walii anakuwa mshirikina.

Miongoni mwa shirki ni kumuomba asiyekuwa Allaah. Mfano mwingine ni du´aa. Akimuomba asiyekuwa Allaah, kwa mfano mtu akamuomba uokozi mwingine asiyekuwa Allaah katika mambo yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah, mtu akaomba ponyo kutoka kwa asiyekuwa Allaah, mtu akaomba kuyaondosha matatizo kutoka kwa asiyekuwa Allaah, mtu huyo anakuwa mshirikina. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufa hali ya kumuomba mwingine asiyekuwa Allaah, basi ataingia Motoni.”[3]

Miongoni mwa aina za shirki ni kuomba msaada, ulinzi na uokozi kutoka kwa mwingine asiyekuwa Allaah. Mtu akaomba msaada kutoka kwa asiyekuwa Allaah katika mambo yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah, mtu akaomba kinga kutoka kwa asiyekuwa Allaah katika mambo yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah au mtu akaomba uokozi kutoka kwa asiyekuwa Allaah katika mambo yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah. Yote haya ni shirki.

Miongoni mwa aina za shirki ni kuwatii viumbe katika kuhalali na kuharamisha. Miongoni mwa ´ibaadah vilevile ni kuwatii viumbe katika kuhalalisha na kuharamisha. Kwa mfano mtu akamtii kiongozi, waziri, mwanachuoni, mfanya ´ibaadah, baba, mke au bosi katika kuhalalisha haramu au kuharamisha halali. Hii pia inakuwa shirki kwa sababu amemfanyia ´ibaadah asiyekuwa Allaah. Kwa sababu Allaah (Ta´ala) ndiye mwenye haki ya kuhalalisha na kuharamisha:

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ

“Je, wanao washirika waliowaamuru dini yale ambayo Allaah hakuyatolea kwayo idhini?”[4]

Mfano mwingine ni mtu kumfanyia Rukuu´ asiyekuwa Allaah, akamfanyia Sujuud asiyekuwa Allaah, akafanya Twawaaf kusipokuwa Ka´bah hali ya kuwa ni mwenye kujikurubisha, akaweka nadhiri kwa mwingine asiyekuwa Allaah, akanyoa kichwa chake kwa ajili ya asiyekuwa Allaah, kama vile Suufiyyah ambapo wamkuta mmoja wao amenyoa kichwa chake kumnyolea Shaykh wake hali ya kuwa ni mwenye kumwabudu. Vivyo hivyo kwa mfano akamfanyia Rukuu´ na Sujuud, akatubu kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah, kama vile Suufiyyah ambao wanatubu kwa ajili ya Mashaykh zao, Shiy´ah ambao wanatubu kwa ajili ya viongozi wao au manaswara ambao wanatubu kwa ajili ya makapadiri wao. Tawbah ni ´ibaadah. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ

“Na nani anayesamehe madhambi isipokuwa Allaah?”[5]

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) pia amepokea kupitia kwa al-Aswad bin Sariy´a ambaye ameeleza kuwa Biasiyr alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambapo akamwambia: “Ee Allaah! Hakika mimi natubia Kwako na situbii kwa Muhammad.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia:

“Itambue haki kwa Mwenye nayo.”[6]

Allaah (Ta´ala) ndiye Mwenye kustahiki kuogopwa na mwenye kusamehe. Allaah (Ta´ala) ndiye mwenye kustahiki kufanyiwa tawbah. Kwa hivyo endapo mtu atatubu kwa mwingine asiyekuwa Allaah ametumbukia katika shirki kwa sababu amemfanyia ´ibaadah asiyekuwa Allaah.

Kwa hivyo mtunzi (Rahimahu Allaah) anasema kuwa kichenguzi cha kwanza ni kufanya shirki katika ´ibaadah ya Allaah. Tumejua kuwa ´ibaadah ni jina lililokusanya kila anachokipenda Allaah na kukiridhia katika maneno na vitendo, ni mamoja vya dhahiri na vilivyojificha. Mtu akifanya aina yoyote ile ambayo imethibiti katika Shari´ah kuwa imeamrishwa, ni mamoja iwe ni maamrisho ya uwajibu au ya kupendeza, au iwe imethibiti katika Shari´ah kuwa imekatazwa, ni mamoja iwe ni makatazo ya uharamu au yanayopendeza, akifanya kitu katika hayo kumfanyia asiyekuwa Allaah anatumbukia katika shirki. Ambaye anamfanyia maamrisho asiyekuwa Allaah au akaacha makatazo kumfanyia asiyekuwa Allaah ametumbukia katika shirki. Mtunzi amepiga mfano wa kuchinja. Mifano mingine ni kama du´aa, kuomba kinga, kuomba uokozi, kuweka nadhiri, Rukuu´, Sujuud, Twawaaf, kutegemea, khofu, matarajio, kunyoa kichwa na mengineyo katika aina za ´ibaadah. Mtu akifanya moja katika mambo haya kumfanyia mwingine asiyekuwa Allaah basi ametumbukia katika shirki na hilo litampelekea katika hukumu zifuatazo:

1 – Hasamehewi.

2 – Mke wake anatengana naye endapo hatotubia papohapo.

3 – Haingii Makkah.

4 – Harithi wala harithiwi.

5 – Haoshwi.

6 – Haswaliwi.

7 – Hatozikwa kwenye makaburi ya waislamu.

8 – Akifa hazikwi pamoja na waislamu kwene makaburi yao.

9 – Kuhusu Aakhirah ni katika watu wa Motoni na Pepo ni haramu kwake.

[1] 06:162-163

[2] 108:02

[3] al-Bukhaariy (4497)

[4] 03:135

[5] Ahmad (03/435)

[6] 42:21

[7] 03:135

[8] Ahmad (03/4357)

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 09/04/2023