06. Adabu ya sita: kuchagua rafiki aliye mzuri


Hakika maimamu (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakichanganyikana na watu na wakiwafunza na wakati huo huo wakiwa ni watu walio na pupa kubwa juu ya kuchunga wakati wao usipotee na usiende bure. Imaam Ahmad (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa ni mtu mwenye subira kubwa juu ya umoja pamoja na kuwa alikuwa ni Imaam wa dini katika wakati wake…

Mwanafunzi anatakiwa kuchanganyika na yule tu ambaye atampa faida au yeye atapata kutoka kwake. Akijipelekea kwa rafiki ambaye anampotezea umri wake kwa kuwa pamoja naye, hamfidishi kitu, hastafidi chochote kutoka kwake, hamsaidii katika lolote, basi aangalie njia nzuri ya kukata ushirikiano wake katika kile kipindi cha mwanzo.

Endapo atahitajia mtu wa kusuhubiana naye, basi mtu huyo awe mwema, mwenye dini, mwenye kumcha Allaah, mnyenyekevu, mwenye kheri nyingi, mwenye shari ndogo, anaposahau anamkumbusha na anapomkumbusha anamsaidia. Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Tambua kwamba si sawa kusuhubiana na kila mtu. Yule unayesuhubiana naye ni lazima awe na sifa zenye kuvutia katika kusuhubiana naye. Yule aliyependekezwa kusuhubiana naye ni lazima awe na sifa tano:

Ya kwanza: Awe na akili.

Ya pili: Tabia njema.

Ya tatu: Asiwe ni mtenda dhambi kubwa.

Ya nne: Asiwe ni mtu wa Bid´ah.

Ya tano: Asiwe ni mwenye kuipupia dunia.

Ni juu ya mwanafunzi akimbilie kujiepusha na yule ambaye haimlazimu kuchanganyika naye Kishari´ah ili aweze kuhifadhi wakati wake na kuutazama moyo wake. Ni juu yake kuchagua rafiki ambaye atamsaidia katika dini na Aakhirah yake.

  • Mhusika: Shaykh Muhammad Sa´iyd Raslaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadab Twaalib-ul-´Ilm, uk. 111-122
  • Imechapishwa: 23/04/2017