05. Wasiwasi wa shaytwaan kwa mwanafunzi

Baadhi ya wanafunzi shaytwaan huwachezea na kuwatia wasiwasi pale wanaposikia mfano wa maandiko kama haya na huwaambia “Ole wenu! Mnaenda wapi? Hamsikii kuwa mnaelekea Motoni? Je, nyinyi hamuukimbii Moto? Mnajipeleka katika maangamivu. Kwenye mioyo yenu kuna kasoro. Haya yatakupelekeeni kutupwa Motoni. Ukimbieni Moto huu. Hakika mimi kwenu ni mwenye kuwanasihi na mwaminifu.” Ibliys anakuwa namna hii hamjii mwanaadamu isipokuwa kwa sura ya mtoaji nasaha mwaminifu ilihali ni khaini na mwongo mkubwa.

Baadhi ya wanafunzi wanaposikia maandiko kama haya anajiwa na shaytwaan kumtia wasiwasi na kumbabaisha. Tahamaki anaacha kujifunza elimu na kujishughulisha na kitu kingine ili awe mwenye kuokoka. Hii ni khasara ya wazi na wakati huo huo ni kumtii shaytwaan. Shaytwaan yuko mbioni kumpoteza ambaye ni mjinga na kuzifanya nyoyo za watu kuwa na giza kutokamana na elimu. Soko la shaytwaan halisimami isipokuwa pindi ujinga unapokita katika soko lake. Mwenendo kama huu kwa mwanafunzi hautakikani.

Pale mwanafunzi anapohisi kasoro fulani ndani ya nafsi yake, basi ajitahidi sana kuitengeneza nia yake na kutafuta njia zitazomsaidia kuitengeneza nia yake. Ajitahidi kuitafuta Ikhlaasw na ajue kuwa kitendo cha kuitafuta Ikhlaasw si sahali na kwamba ni jambo linahitajia subira kubwa na kuwa anahitajia matibabu makubwa. Anatakiwa amuombe Allaah (´Azza wa Jall) Ikhlaasw katika Sujuud yake na katika hali zake zote. Amuombe Allaah (´Azza wa Jall) amtakase kutokamana na shari, amruzuku kheri, amweke pamoja na watu wa Ikhlaasw, ajitahidi katika kufanya ´ibaadah na kutenda ´amali. Hakika kufanya ´ibaadah ni sababu ya kuzidi kwa imani. Imani ya mja ikizidi moyo wake utanyooka, matendo yake yatakuwa mema na atamkaribia Mola Wake. Kwa kufanya hayo atakaribia kuwa ni mwenye kumtakasia nia Allaah katika kusoma kwake.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016