05. Sunnah ni Wahy kutoka kwa Allaah kama ilivyo Qur-aan

Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wameihifadhi Sunnah zake za kimaneno na za kimatendo na wakawafikishia Taabi´uun waliokuja baada yao, Taabi´uun wakawafikishia waliokuja baada yao na vilevile wanachuoni waaminifu wakainukuu kizazi baada ya kizazi na karne baada ya karne. Waliikusanya katika vitabu vyao, wakaweka wazi ambazo ni Swahiyh na mbovu. Wakaweka baina yao kanuni na vidhibiti vya kuyajua hayo. Kupitia kanuni na vidhibiti hivyo inapata kujulikana Hadiyth Swahiyh na dhaifu. Wanachuoni wametunga vitabu vya Sunnah – kama mfano wa “as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy na “as-Swahiyh” ya Muslim – na wakaihifadhi kikamilifu kama ambavyo Allaah amekihifadhi Kitabu Chake kitukufu kutokamana na michezo ya wachezaji, ukafiri wa makafiri na upotoshaji wa wapotoshaji. Hilo ni kwa kuhakikisha maneno Yake (Subhanaah):

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

“Hakika Sisi ndio tumeteremsha Ukumbusho na hakika Sisi bila shaka ndio tutakaoihifadhi.” (15:09)

Hapana shaka kwamba Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Wahy wenye kuteremshwa. Allaah ameihifadhi Sunnah pia kama alivyohifadhi Kitabu cha Allaah na akaifanya kuwa na wanachuoni wakosoaji ambao wanaraddi upotoshaji wa wapotoshaji, tafsiri za kimakosa za wajinga na wakailinda na yale yote wajinga, waongo na wakanamungu wanayojaribu kuyapenyeza ndani yake. Hilo ni kwa kuwa Allaah (Subhaanah) ameifanya kuwa ndio tafsiri ya Kitabu Chake kitukufu na kubainisha zile hukumu zilizokuja kwa jumla. Vilevile katika Sunnah kuna hukumu nyenginezo ambazo hazikutajwa na Qur-aan. Mfano wa hizo ni hukumu za unyonyeshaji, baadhi ya hukumu za mirathi, kumuoa mwanamke na shangazi yake na mwanamke, khale yake[1] kwa wakati mmoja na hukumu nyenginezo ambazo zimekuja katika Hadiyth Swahiyh na hazikutajwa katika Qur-aan. Tutataja baadhi ya yaliyothibiti kutoka kwa Maswahabah, Taabi´uun na waliokuja baada yao kuhusu kuiadhimisha Sunnah na uwajibu wa kuitendea kazi.

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema: “Pindi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokufa waliritadi baadhi ya mabedui ambapo Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) akasema: “Ninaapa kwa Allaah! Nitampiga vita yule mwenye kutofautisha kati ya swalah na zakaah.” ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) akamwambia: “Vipi utawapiga vita ilihali Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Nimeamrishwa kuwapiga watu vita mpaka waseme ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`. Wakifanya hivo basi imesalimika kwangu damu na mali yao isipokuwa kwa haki yake.” Abu Bakr as-Swiddiyq akasema: “Kwani zakaah sio katika haki yake? Ninaapa kwa Allaah wakizuia kitu walichokuwa wakitoa katika zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nitawapiga vita kwa kukizuia kwao.” ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) anasema: “Nilikuja kujua kuwa ni haki pale nilipoona kuwa Allaah amekifungua kifua cha Abu Bakr juu ya vita na Maswahabah wakamfuata katika hilo. Hivyo akawapiga vita walioritadi mpaka wakarudi katika Uislamu na wakauawa wale walioendelea kung´ang´ania juu ya kuritadi kwao.”

Katika kisa hiki kuna dalili ya wazi juu ya kuiadhimisha Sunnah na uwajibu wa kuitendea kazi.

[1] Mamdogo, dada ya mama.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ujuwb-ul-´Amal bis-Sunnah
  • Imechapishwa: 23/10/2016