05. Sharti za wudhuu´


Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Unakuwa ni wajibu wakati wa hadathi na sharti zake ni kumi:

1-  Uislamu.

2- Kuwa na akili.

3- Kuweza kupambanua.

4- Nia.

5- Mtu asinuie kuukata [wudhuu´ wake] mpaka atakapomaliza kutawadha.

6- Kukatika kwa yale yanayowajibisha wudhuu´.

7- Kujisafisha kwa maji au kwa kutumia mawe kabla yake.

8- Maji yawe masafi na yasiwe ma madhara.

9- Maji yawe yenye kuruhusiwa/ya halali.

10- Kuondosha kila kinachozuia maji kufika kwenye ngozi.

Kuingia kwa wakati wa kile kitendo cha faradhi kwa yule ambaye daima yuko katika hali ya hadathi.

MAELEZO

Wudhuu´ hausihi isipokuwa mpaka kwa kutumia sharti kumi. Baadhi yake ni Uislamu, akili na kupambanua. Ili mtu aweze kujitawadha anatakiwa awe muislamu, awe na akili na awe na uwezo wa kupambanua mambo.

Sharti ya nne ni nia. Anatakiwa kunuia twahara baada ya hadathi ambayo amepata kutokana na kukojoa, kutokwa na upepo au kichenguzi kingine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika kila kitendo kinategemea na nia na kila mmoja atalipwa kwa kile alichonuia.”[1]

Sharti ya tano ni kwamba anatakiwa kubaki na nia mpaka pale atapomaliza kutawadha. Hili linahusu swalah na wudhuu´. Ni lazima aendelee kuwa na nia mpaka pale atapomaliza kutawadha. Aendelee na nia na asiikate mpaka pale atapomaliza wudhuu´ wake. Kwa mfano akiosha uso na mikono yake kisha akanuia kuukata na kurudi kutawadha tena, basi analazimika kurudi kutawadha kuanzia mwanzo. Kwa sababu wudhuu´ wake umekatika pale alipokata nia yake.

Sharti ya sita ni kukatika kwa yale yote yanayowajibisha wudhuu´. Anatakiwa kutawadha baada ya kukatika yale yote yanayowajibisha wudhuu´. Kwa mfano mkojo au kutokwa na kinyesi. Si sahihi kutawadha na huku mkojo unamtoka. Kwanza unatakiwa mkojo kukatika kisha baadaye ndio atawadhe.

Sharti ya saba kujisafisha kwa maji au kwa kutumia mawe kabla ya kutawadha. Baada ya kupata hadathi kwa kukojoa au kujisaidia haja kubwa anatakiwa kujisafisha kwa maji au kwa kutumia mawe. Anatakiwa kujisafisha kwa maji au kwa mawe chini chini mara tatu. Kupangusa kunatakiwa kuwe chini chini mara tatu na sehemu hiyo kusafike.

Sharti ya nane maji yawe masafi.

Sharti ya tisa maji yawe yenye kuruhusiwa. Kwa msemo mwingine yasiwe yaliyochukuliwa kwa mabavu wala ya haramu. Swali: Je, wudhuu´ unasihi katika chombo cha dhahabu na fedha? Haijuzu kutumia vyombo vya dhahabu na vya fedha. Kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuvitumia. Lakini hata hivyo kutawadhia ndani  yavyo kunasihi pamoja na kuwa ni haramu. Kwa sababu lengo limefikiwa. Baadhi ya wanachuoni wamekataza hilo – na hayo ndio maoni ya mwandishi. Kutumia vyombo vya dhahabu na vya fedha haviruhusiwi kwa sababu ni kama vyombo vilivyoporwa. Havisihi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kufanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu basi atarudishiwa mwenyewe.”

Wale ambao wanaonelea kuwa umesihi wamesema kwamba lengo ni twahara na tayari imekwishapatikana kwa maji na wanaonelea kuwa dhambi haizuii. Ni kama mtu akijitupa kwenye bwawa na akatawadha pasi na kupewa idhini na mwenye nayo, akafanya Tayammum kwenye udongo wa ardhi ya watu pasi na kupata idhini yao na mfano wa hayo. Lengo ni ile twahara na tayari imekwishapatikana. Kupata kwake dhambi kwa kule kutumia kitu ambacho hafai kwake kukitumia hakuzuii kusihi kwa wudhuu´. Kilichokatazwa ni kitendo kitendo cha kupora na dhuluma na sio wudhuu´. Lakini lililo salama zaidi kwa muumini ni yeye arudi kutawadha upya na ajiweke mbali na mambo ambayo wanachuoni wametofautiana. Ahakikishe hatawadhi isipokuwa kwa kutumia maji yaliyoruhusiwa. Kwa ajili hiyo ndio maana mwandishi amekata ya kwamba kuruhusiwa kwa maji ni sharti ya kusihi kwa swalah kwa kutumia msingi unaosema:

“Yale niliyokukatazeni basi jiepusheni nayo… “

Sharti ya kumi kuondosha kila kinachozuia maji kufika kwenye ngozi. Akiwa na unga au kitu kingine mikononi au usoni kinachozuia maji kufika kwenye ngozi, basi anatakiwa kukiondosha kwanza.

Sharti ya kumi na moja ni kuingia kwa wakati wa kile kitendo cha faradhi kwa yule ambaye daima yuko katika hali ya hadathi. Mfano wa watu hao ni mwanamke anayetokwa na damu ya ugonjwa au mtu anayetokwatokwa na mkojo hovyo. Watu hawa wanatakiwa kutawadha baada ya kuingia wakati. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia mwanamke mwenye kutokwa na damu ya ugonjwa:

“Tawadha kila kunapoingia wakati wa kila swalah.”[2]

[1] al-Bukhaariy (1) na Muslim (1907).

[2] Abu Daawuud (298), at-Tirmidhiy (128) na Ahmad (6/382).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumtaaz, uk. 64-66
  • Imechapishwa: 25/06/2018